Serikali kupitia kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa imemuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Camillus Wambura kulisimamia Jeshi hilo ili kufanya ukaguzi wa vyombo vya moto barabarani, kuimarisha doria usiku na mchana pamoja na kuimarisha ulinzi kwenye Nyumba za Ibada katika kipindi hiki cha kuelekea sikukuu za Christmas na Mwaka Mpya.
Bashungwa ametoa maagizo hayo wakati akitoa taarifa kwa Umma kuelekea Sikukuu za Mwisho wa Mwaka ambapo amewahakikishia Watanzania wote kuwa nchi iko salama.
“Hatuko tayari kuacha tabia za kizembe ziendelee kupoteza maisha ya watu, na wengine kupata ulemavu, huku Sheria za kudhibiti uzembe zikiwa zipo.Tutachukua hatua kali kwa madereva na wasafarishaji wazembe.
Ninaomba wasafiri mtupe ushirikiano, na kuunga mkono jitihada hizi, ili tuwe salama tunapokuwa barabarani”amesema Bashungwa.
Bashungwa ametoa wito kwa wasafiri na wasafirishaji, kuzingatia na kuheshimu Sheria za Usalama Barabarani, ili kupunguza ajali zinazoepukika ambazo zimekuwa zikisababisha vifo, majeruhi na hata kusababisha ulemavu kwa wananchi.
“Nitoe tahadhari kwa familia zinazotumia magari yao binafsi, kufanya matengenezo ya magari kabla ya safari, na kuacha utamaduni wa kuchukua mtu yeyote ambaye hana taaluma ya udereva, wala leseni, na hajapitia mafunzo ya kuendesha magari kwa kukwepa gharama. Kila familia ichukue tahadhari, hususani tunapoelekea mwisho wa mwaka.”
Kadhalika, Bashungwa amemuagiza IGP Camillus Wambura na Jeshi la Polisi kwa ujumla kuendelea na operesheni Maalum katika mikoa yote nchini ya kupambana na wezi na wahujumu wa miundombinu ya TANESCO, SGR, barabara na miundombinu mingine na watuhumiwa wanaokamatwa, upelelezi ukamilike mapema na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Ametoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari kubwa katika maeneo yenye mikondo ya maji inayokatiza barabarani pamoja na wazazi na walezi kutoacha watoto kuvuka pekee yao kwenye maeneo hatarishi ya maji au kuogelea kwenye madimbwi kutokana na mvua nyingi zinazoendelea kunyesha katika baadhi ya maeneo nchini.
“Upo utamaduni kwenye sherehe za mwisho wa mwaka, wazazi kuwaacha watoto kwenda sehemu mbalimbali kwa ajili ya kusherehekea sikukuu, yakiwemo maeneo ya ufukweni au kwenye maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya michezo ya watoto, huku wakiwa peke yao. Niwaombe wazazi kuwalinda watoto na kutoruhusu watoto kwenda kutembea siku za sikukuu wakiwa peke yao” amesisitiza
Pia, Bashungwa ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kumuombea Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuipa ushirikiano Serikali ili kuifanya nchi kuendelea kuwa katika hali ya amani na utulivu, na kuwafanya wananchi kushiriki katika shughuli za kiuchumi na kijamii.
#KhomeinTvUpdates
✍️Mwandishi wetu
PIA USIACHE KU SUBSCRIBE
CHANEL YETU Khomein TV
YOUTUBE UWE WA KWANZA
KUFIKIWA NA HABARI ZETU
Follow Insta & Threads @khomeintv_
Tufollow pia kwenye X (Twitter), TikTok
@khomeintv na Facebook Khomein Tv
0 Comments