SERIKALI YA SAMIA YAWAONYA WATUMISHI WAZEMBE

 

Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, imewaonya watumishi wazembe kuacha tabia hiyo na kutaka wabadilike haraka.

 

Naibu Waziri wa wizara hiyo Deus Sangu amesema ajira ya kudumu Serikalini imekuwa ikisababisha watumishi wa umma kuwa wazembe na kukaa bila kufanya kazi wakiamini ikifika mwisho wa mwezi watapata mshahara jambo ambalo ni kinyume cha Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma.

 

Sangu ametoa kauli hiyo wiki hii jijini Dodoma wakati akifunga kikao kazi cha siku tatu cha  Wakuu wa Idara za Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma.

 

Amesema masharti ya ajira ya kudumu na mafao Serikalini kwa Watumishi wa Umma yanawaharibu watumishi ambapo wamejikuta wakifanya kazi kwa mazoea bila kuchukuliwa hatua licha ya kukiuka Sheria, Taratibu na Kanuni jambo ambalo linaweza kuisababishia serikali hasara kubwa.

 

Amesema katika ziara aliyoifanya kwenye baadhi ya mikoa amebaini changamoto hizo hasa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ambapo kuna baadhi ya maeneo amekuta Watendaji wa Kata na Vijiji wakifanya kazi kama miungu watu bila kuchukuliwa hatua za nidhamu licha ya kulewa asubuhi mpaka jioni huku wananchi wakikosa huduma.

 

"Nimefika moja ya eneo ambalo Mtendaji wa Kijiji na Kata analewa kuanzia asubuhi mpaka jioni siku zote za kazi, wananchi wanahitaji huduma hawapati, ukimuuliza mwajiri anasema ndio kawaida yake tumeshamzoea, katika utumishi wa umma hakuna mazoea ya namna hiyo na haikubaliki hata kidogo," amesema Sangu.

 

Pia, alizitaja changamoto nyingine alizokutana nazo katika maeneo hayo kuwa ni uzembe, vitendo vya rushwa, ulevi uliokithiri, kutoa  lugha zisizofaa, unyanyasaji, uonevu na ubinafsi hasa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, kutopandishwa vyeo, kutolipa malimbikizo ya mishahara, na suala la uhamisho.

 

Amesema, wamebaini kuwa changamoto zote hizo zimesababishwa na watumishi wazembe, wabinafsi na wasiotaka kuwajibika kwa weledi katika utekelezaji wa majukumu yao.

 

#KhomeinTvUpdates 

 

️Mwandishi wetu

 

PIA USIACHE KU SUBSCRIBE

CHANEL YETU Khomein TV

YOUTUBE UWE WA KWANZA 

KUFIKIWA NA HABARI ZETU

 

Follow Insta & Threads @khomeintv_

Tufollow pia kwenye X (Twitter), TikTok

@khomeintv na Facebook Khomein Tv

Post a Comment

0 Comments