Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameondoka nchini kuelekea Addis Ababa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia, kushiriki Mkutano wa 39 wa Kawaida wa Baraza la Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU), utakaofanyika Februari, 14 na 15 2026.
Kabla ya mkutano huo, Rais Samia anatarajiwa kushiriki kikao cha Kamati ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (CAHOSCC), kitakachoandaliwa na William Samoei Ruto, Rais wa Jamhuri ya Kenya.
Baada ya hapo, atahudhuria Dhifa ya Kitaifa iliyoandaliwa kwa heshima yake na Abiy Ahmed Ali, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia.
Kando ya Mkutano huo, Rais Samia pia amepangiwa kufanya mikutano ya ngazi ya juu ya pande mbili na viongozi mbalimbali, akiwemo Waziri Mkuu wa Ufalme wa Eswatini Russell Mmiso Dlamini, Azali Assoumani, Rais wa Muungano wa Komoro na Bi. Amina Mohammed, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika na Dkt. Sidi Ould Tah.
Mikutano hiyo inalenga kuimarisha mazungumzo ya kisiasa, kukuza ushirikiano wa kiuchumi, na kusukuma mbele vipaumbele vya maendeleo vya pamoja.
Mkutano huo utaanza rasmi tarehe 14 Februari 2026 chini ya kaulimbiu, “Kuhakikisha Upatikanaji Endelevu wa Maji na Mifumo Salama ya Usafi wa Mazingira ili Kufikia Malengo ya Ajenda 2063,” Ikiakisi azma ya pamoja ya Nchi Wanachama kuimarisha usalama wa maji, kukuza afya ya umma, na kuharakisha maendeleo endelevu na jumuishi barani Afrika.
Tanzania inahitimisha muda wake wa uanachama katika Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika, baada ya kuhudumu kwa vipindi viwili mfululizo kuanzia mwaka 2022 hadi 2026.
Katika kipindi hicho, Tanzania imetoa mchango mkubwa na wa kujenga katika juhudi za bara zenye lengo la kuimarisha amani, utulivu, kuzuia migogoro, na kujenga upya baada ya migogoro.
Baraza la Wakuu wa Nchi na Serikali ndilo chombo cha juu cha maamuzi cha Umoja wa Afrika, chenye mamlaka ya kupitisha maazimio yanayofunga na kutoa mwelekeo wa kisiasa wa kimkakati kuhusu vipaumbele muhimu vya bara, ikiwemo amani na usalama, ushirikiano wa kiuchumi, maendeleo endelevu, mageuzi ya taasisi, na utekelezaji wa Ajenda 2063.
#KhomeinTvUpdates
0 Comments