SERIKALI YAAGIZA MIRADI YA UJENZI BRT KUKAMILIKA KABLA YA MVUA

 

Serikali ya awamu ya Sita, chini ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeazimia kusimamia kikamilifu Miradi yake ya maendeleo, ambapo imeagiza miradi ya ujenzi wa miundombinu ya Mabasi yaendayo Haraka (BRT), ikamilike kabla ya msimu wa mvua za Masika mapema mwakani ili kupunguza changamoto za msongamano wa magari katika Jijini Dar es Salaam.

 

Katika kutekeleza azma hiyo, Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega, amefanya ziara ya kushtukiza usiku wa kuamkia Disemba 28, 2024 yenye lengo la kukagua maendeleo ya miradi hiyo ya (BRT) katika maeneo mbalimbali Jijini Dar es Salaam.

 

Katika ziara hiyo, Waziri Ulega ameagiza miradi hiyo ikamilike haraka, kazi ifanyike usiku na mchana ili kuhakikisha miradi hii inakamilika kwa wakati,”amesema Waziri Ulega. 

 

“Msimu wa mvua za masika una changamoto zake, na hatutaki kuona wananchi wakitaabika, tunafanya hivi kwa kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais pamoja na Ilani ya CCM  ya  2020-2025, inayosisitiza kupunguza msongamano wa magari mijini," amesema Waziri Ulega.

 

Katika ziara yake hiyo , Waziri Ulega amekagua maendeleo ya upanuzi wa barabara ya BRT 1 kutoka Ubungo hadi Kimara pamoja na barabara ya Mwenge kuelekea Tegeta inayojumuishwa katika mradi wa BRT 4.

 

Amesema, ameridhishwa na kasi ya kazi zinazofanywa na wakandarasi ambao wameanza kutekeleza agizo lake la kufanya kazi saa 24 kila siku.

 

"Timu ya usimamizi ya TANROADS chini ya Mtendaji Mkuu wake, Mhandisi Mohamed Besta, inafanya kazi nzuri, Wakandarasi lazima wafanye kazi muda wote bila kupoteza muda,” amesisitiza.

 

Amesema, Watanzania wanatamani kuona miradi hii ikikamilika, na Serikali inajali maslahi yao.

 

Kwa upande wake, Mhandisi Mohamed Besta amemhakikishia Waziri kuwa TANROADS itaendelea kusimamia wakandarasi kwa karibu ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati.

 

"Tutaendelea kufanya hivi kusimamia wakandarasi kufanya kazi usiku na mchana,  hata pale ambapo Mhe. Waziri wa Ujenzi hautakuja kufanya ziara za kushtukiza, tutahakikisha kazi inaendelea kwa kasi ili kufanikisha lengo la kupunguza msongamano wa magari Jijini Dar es Salaam," amesema Mhandisi Besta.

 

Meneja wa Mradi wa BRT, Mhandisi Allen Natai, ameeleza kuwa kazi ya kujenga miundombinu ya barabara za mabasi yaendayo haraka inaendelea vizuri.

 

Ziara ya Waziri Ulega imeonyesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha miradi mikubwa ya maendeleo inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa ili kuboresha huduma kwa wananchi na pia imetoa msukumo mpya kwa utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya Mabasi yaendayo Haraka (BRT) Jijini Dar es Salaam.

 

️ Mwandishi wetu

 

PIA USIACHE KU SUBSCRIBE

CHANEL YETU Khomein TV

YOUTUBE UWE WA KWANZA 

KUFIKIWA NA HABARI ZETU

 

Follow Insta & Threads @khomeintv_

Tufollow pia kwenye X (Twitter), TikTok

@khomeintv na Facebook Khomein Tv

Post a Comment

0 Comments