Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani Mwalimu Hassan Nyange, amesema ataanza kulipa fedha ya motisha shilingi 400,000 kwa mwezi, wanafunzi 8 wenye ulemavu wanaosoma sekondari ya Ufundi Mtwara kwa kumpa shilingi 50,000 kila mmoja, pamoja na mkalimani wao ambaye atamlipa shilingi 300,000 kila mwezi.
Mwalimu Nyange, ameeleza hayo leo Januari 27, 2025 katika Kongamano la Elimu kwa Wanafunzi wa Kidato cha Nnne, lililofanyika kwenye viwanja vya Mashujaa Manispaa ya Mtwara-Mikindani, ambapo mgeni rasmi alikua Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala.
Kongamano hilo lililohusisha zaidi ya wanafunzi 200 wa kidato cha Nne kutoka shule zote za Sekondari ndani ya Manispaa hiyo, limelenga kuwapa motisha wanafunzi hao kuelekea mitihani yao ya kuhitimu kidato cha Nne pamoja na kuhakikisha manispaa hiyo inafuta daraja sifuri kwenye matokeo ya kidato cha Nne.
Katika mahojiano yake na wanahabari baada ya Kongamano hilo, Mkurugenzi Mwalimu Hassan Nyange, amesema sekondari ya Mtwara Ufundi imeongoza kufaulisha Kitaifa kwa kushika nafasi ya kwanza kwa shule za Ufundi, huku kwa mara ya kwanza ikifuta daraja sifuri kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu.
“Kwahiyo watoto wenye ulemavu wale mimi nawalea, wapo Nane wale tunawapa sapoti kwasababu wengi wanatoka familia duni, wana mahitaji mmewaona yule anayetembezwa kwenye kiti kwamfano, kwahiyo wale kila mwisho wa mwezi hela yangu mimi yani Elfu Hamsini mara Nane ni laki ngani si Laki Nne, siwezi kukosa mimi Laki Nne ya pepo kesho.” Amesema Nyange.
Akizungumzia motisha hiyo, Mwanafunzi Benjamin Magigi, ambaye ni mkalimani wa lugha ya alama anayefanya kazi ya kutafsiri kwa wanafunzi hao, ambaye ameahidiwa kupewa shilingi 300,000 kila mwezi, amesema itamsaidia kwenye mahitaji yake shuleni hapo.
“Hii kitu kwa uande wangu ninaichukua kwa furaha sana kwasababu ni kama chanzo cha ajira kwangu kwasababu toka naanza nilikuwa nikifanya kwa moyo..” Ameeleza Magigi.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala, akawaeleza wanafunzi hao umuhimu wa kusoma kwa bidii na kuachana na dhana ya kuaminishwa kuwa hakuna ajira.
“Nawaambieni wanangu hasiwadanganye mtu, kuna watu watakuja kuwaambia aah! Hakuna ajira, sijui nini kama ni mtoto wa kike atakuambia nenda kaolewe anakudanya.” Kanali Sawala.
Mkuu wa wilaya ya Mtwara Abdallah Mwaipaya, amesema “ni lazima tuwe na mambo matatu, Nidhamu, Bidii na Uvumilivu kwasababu mafanikio hua hayaji kama upepo hivi au kama maji, mafanikio yanakuja kutokana na bidii lakini pia nidhamu. Kama hauna hivi vitu, hauna bidii, hauna nidhamu hakuna kitu ambacho unaweza ukafanikiwa.” Amesisitiza Mwaipaya.
Katika kongamano hilo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara akawaongoza viongozi kukata keki kwa ajili ya kumpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kusherehekea siku ya kumbukizi ya kuzaliwa.
Katika matokeo ya kidato cha nne mwaka huu, Manispaa ya Mtwara-Mikindani imeshika nafasi ya kwanza kwa ufaulu, kwa mkoa wa Mtwara, huku sekondari ya Mtwara Ufundi ikiongoza Kitaifa kwa sekondari za Ufundi.
#KhomeinTvUpdates
✍️ Juma Mohamed-Mtwara
PIA USIACHE KU SUBSCRIBE
CHANEL YETU Khomein TV
YOUTUBE UWE WA KWANZA
KUFIKIWA NA HABARI ZETU
Follow Insta & Threads @khomeintv_
Tufollow pia kwenye X (Twitter), TikTok
@khomeintv na Facebook Khomein Tv
0 Comments