Serikali ya Awamu ya Sita inayongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imemtaka mkandarasi wa ujenzi wa uwanja wa ndege wa Shinyanga afanye kazi usiku na mchana ili kuhakikisha anakamilisha ujenzi wa uwanja huo ikiwemo ufungaji wa taa na uanze kutumika wakati wote.
Ukaguzi huo umefanywa Jumapili Februari 16, 2025 na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipokagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa uwanja wa ndege wa Shinyanga ambao kwa ujumla ujenzi wake umefikia Asilimia 73.9.
Majaliwa amesema kuwa uwanja huo ni wa kimkakati uliokuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu na wakazi wa mkoa wa Shinyanga na maeneo ya jirani ikiwemo mkoa wa Simiyu.
“CHICO tunajua unafanya kazi nzuri, hapa kasoro yako unachelewesha kuingiza vifaa vilivyobaki, Meneja wa TANROAD ameniambia mmekamilisha kwa asilimia 100 kwenye eneo la kuruka na kutua ndege, sio kweli, bado taa, kwa hiyo agiza taa mara moja zije hapa, tunaweza kuutumia uwanja wetu usiku, hata kama jengo halijakamilika, mnaweza kutumia jengo la zamani, hamdai chochote fedha zote mmelipwa”
Amesema kuwa dhamira ya Serikali ya kuendelea kuimarisha Sekta ya usafirishaji ni dhamira kamili na kwa sasa inatekelezwa kwa vitendo “Leo hii kila mkoa tuna uwanja wa ndege ukiondoa mikoa mipya ikiwemo Simiyu lakini Serikali inaendelea na ujenzi katika maeneo hayo”
Aidha, Majaliwa amewataka Watanzania waliofanya kazi za ujenzi kwenye uwanja wa ndege wa Shinyanga kutumia uzoefu na ujuzi walioupata kujiendeleza na ikiwezekana kuanzisha makampuni ya ujenzi ili kunufaika na miradi mingine itakayotolewa na Serikali.
Naye, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Patrobas Katambi amemshukuru Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika mkoa huo ikiwemo ujenzi wa uwanja wa ndege.
“Leo tumeweka uwanja wa ndege kwenye eneo hili uliogharimu shilingi bilioni 49, tunamshukuru sana Rais Dkt. Samia”
Kwa Upande wake Meneja wa TANROAD mkoa wa Shinyanga Mhandisi Samwel Mwambungu Amesema kuwa Serikali katika kuhakikisha inaendelea kuboresha usafiri wa anga kwa mkoa wa Shinyanga, iliingia mkataba na mkandarasi kutoka China (CHICO) kwa gharama ya Shilingi bilioni 49.2 kwa ajili ya ujenzi na upanuzi wa uwanja wa ndege wa Shinyanga.
Amesema kuwa Mradi ulihusisha ujenzi wa njia ya kurukia ndege yenye urefu wa mita 2.2 na upana wa mita 30, ujenzi wa jengo la abiria lenye uwezo wa kuhudumia abiria 250,000 hadi 300,000 kwa mwaka na abiria 120 kwa wakati mmoja.
Maeneo mengine ni usimikaji wa taa za kuongozea ndege, ujenzi wa mitaro ya maji, uzio kuzunguka kiwanja, barabara ya mzunguko ndani ya kiwanja na barabara za kufikia kwenye uwanja wa ndege.
#KhomeinTvUpdates
✍️Mwandishi wetu
PIA USIACHE KU SUBSCRIBE
CHANEL YETU Khomein TV
YOUTUBE UWE WA KWANZA
KUFIKIWA NA HABARI ZETU
Follow Insta & Threads @khomeintv_
Tufollow pia kwenye X (Twitter), TikTok
@khomeintv na Facebook Khomein Tv
0 Comments