Mtandao wa barabara zinazohudumiwa na TANROADS waongezeka, miradi mikubwa ya ujenzi yakamilika
Katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, sekta ya ujenzi imepiga hatua kubwa na kuonesha mafanikio ya wazi katika kuboresha miundombinu ya nchi. Mafanikio haya ni matokeo ya mikakati madhubuti ya Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, sambamba na usimamizi imara wa miradi mikubwa ya kimkakati.
Moja ya mafanikio makubwa ni kukamilika kwa ujenzi wa Daraja la Kigongo–Busisi, linalojulikana rasmi kama Daraja la JP Magufuli, lenye urefu wa kilomita 3. Daraja hilo ambalo sasa lina uwezo wa kupitisha zaidi ya magari 20,000 kwa siku, limefungua fursa mpya za kiuchumi na kijamii kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa, hususan mikoa ya Mwanza na Geita, kwa kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji wa bidhaa.
Akizungumza jijini Mwanza Juni 8, 2025 wakati wa kutangaza mafanikio ya sekta hiyo, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ameeleza kuwa Rais Samia alipoingia madarakani mwaka 2021, utekelezaji wa mradi huo ulikuwa umefikia asilimia 25 pekee. Hata hivyo, katika kipindi kifupi cha miaka minne, Serikali imefanikisha kukamilika kwa ujenzi huo kwa asilimia 100.
Waziri Ulega ameendelea kufafanua kuwa mtandao wa barabara unaohudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) umeongezeka kutoka kilomita 36,361.95 hadi 37,435.04, ikiwa ni ongezeko la kilomita 1,073.09. Ongezeko hili linatokana na baadhi ya barabara kupandishwa hadhi na kutambuliwa kama barabara za Kitaifa.
Aidha, katika kipindi hicho, jumla ya kilomita 15,511.25 za barabara zipo katika hatua mbalimbali za ujenzi, hatua inayolenga kuimarisha mtandao wa miundombinu ya barabara nchini kote.
Katika juhudi za kupunguza msongamano wa magari mijini, Serikali imekamilisha ujenzi wa madaraja makubwa 8, huku madaraja mengine 12 yakiendelea kujengwa katika maeneo mbalimbali ya nchi. Mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza na Mbeya imetajwa kuwa kati ya maeneo yanayonufaika na mikakati hii, ambayo inalenga kuboresha huduma za usafiri mijini, kupunguza muda wa kusafiri, na gharama za uendeshaji wa magari.
Waziri Ulega pia ameeleza kuwa Serikali imejikita katika kulinda ubora wa barabara kwa kusimamia matumizi ya mizani za kisasa. “Tunaweka ulinzi wa barabara hizi kwa kujenga mizani za kisasa zenye matumizi kidogo ya binadamu, kufunga mizani za kielektroniki zinazopima magari yakiwa katika mwendo, pamoja na mifumo ya CCTV katika vituo vyote vya mizani ifikapo mwaka 2027,” amefafanua.
Hatua hizi zote ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa nafasi mtandao wa barabara wa kisasa, salama, na wa kuaminika, ambao unachochea ukuaji wa uchumi wa nchi kwa ujumla.
#KhomeinTvUpdates
✍️Juma Mohamed-Dar
PIA USIACHE KU SUBSCRIBE
CHANEL YETU Khomein TV
YOUTUBE UWE WA KWANZA
KUFIKIWA NA HABARI ZETU
Follow Insta & Threads @khomeintv_
Tufollow pia kwenye X (Twitter), TikTok
@khomeintv na Facebook Khomein Tv
0 Comments