RASILIMALI MAJI NI USALAMA WA TAIFA — WAZIRI AWESO

 

Waziri wa Maji, Juma Aweso, amesema kuwa uwepo wa Wizara ya Maji unategemea moja kwa moja uwepo wa rasilimali za maji, na kwamba maji ya kutosha ni msingi wa usalama wa Taifa. Kwa mujibu wake, upatikanaji wa maji ya kutosha huleta uhakika wa chakula, nishati, na utekelezaji wa mipango yote ya maendeleo.

 

Kauli hiyo ameitoa Dodoma, Juni 2, 2025 wakati wa hafla ya Ufunguzi wa Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ambayo Kitaifa yanafanyika jijini Dodoma kuanzia Juni 1 hadi Juni 5, 2025. Kaulimbiu ya mwaka huu ni: “Mazingira Yetu na Tanzania Ijayo, Tuwajibike Sasa; Kuthibiti Matumizi ya Plastiki.”

 

Waziri Aweso amesema Wizara ya Maji itaendelea kushirikiana kwa karibu na wadau wote wa mazingira katika kulinda na kutunza mazingira, kwa lengo la kuhakikisha Tanzania inabaki kuwa nchi salama na yenye ustawi endelevu. Amebainisha kuwa tayari Wizara imefanya marekebisho ya sera ili ziendane na hali halisi ya sasa na kuruhusu ushirikiano mpana na wadau mbalimbali.

 

Aidha, amewataka Watanzania kujifunza kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira, akisema kwamba madhara hayo ni dhahiri. Ametoa mfano wa Mto Ruvu ambao ulionekana kukauka miaka miwili iliyopita, hali aliyoieleza kuwa ni matokeo ya moja kwa moja ya shughuli za kibinadamu, na siyo mabadiliko ya tabianchi pekee.

 

Vilevile, Waziri Aweso ameelezea athari za kilimo katika vyanzo vya maji pamoja na ukataji miti hovyo, akisisitiza kuwa vitendo hivyo vina madhara makubwa. Ametoa mfano wa eneo la Pangani mkoani Tanga, ambako kina cha bahari kimeongezeka na kuathiri maeneo ya mji, ikiwa ni ishara ya mabadiliko ya mazingira.

 

Pia, ameipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais ambao ndio wenyeji wa maonesho hayo, kupitia Idara ya Mazingira kwa kuweka mikakati madhubuti ya kulinda mazingira nchini. Sambamba na hilo amemtaja Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kama kiongozi shupavu aliyeweka ajenda ya mazingira kuwa kipaumbele katika uongozi wake.

 

#KhomeinTvUpdates 

 

✍️Mwandishi wetu

 

PIA USIACHE KU SUBSCRIBE

CHANEL YETU Khomein TV

YOUTUBE UWE WA KWANZA 

KUFIKIWA NA HABARI ZETU

 

Follow Insta & Threads @khomeintv_

Tufollow pia kwenye X (Twitter), TikTok

@khomeintv na Facebook Khomein Tv

Post a Comment

0 Comments