Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imeendelea kuonesha uthabiti na weledi katika kusimamia masuala ya usafiri wa umma nchini, hasa katika kipindi hiki cha majaribio ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) kwenye njia ya Mbagala–Gerezani jijini Dar es Salaam.
Katika ziara maalum iliyofanyika Jumamosi Oktoba 18, 2025, Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, CPA Habibu Suluo, aliongoza timu ya wataalamu kukagua mwenendo wa huduma hiyo, lengo likiwa ni kutathmini ubora, ufanisi na uhalisia wa gharama za uendeshaji kabla ya mfumo huo kuanza rasmi.
Kwa mujibu wa maelezo ya Suluo, LATRA haibahatishi katika majukumu yake ya udhibiti. Ameweka wazi kuwa nauli ya sasa ya shilingi 750 itaendelea kutumika hadi pale mwekezaji atakapokamilisha vigezo vyote vilivyowekwa, ikiwa ni pamoja na kushughulikia changamoto za kiufundi, miundombinu na mfumo wa malipo.
“Tunataka huduma hii iwe ya uhakika, salama na yenye ufanisi kwa wananchi wote. Tutahakikisha kila changamoto inatatuliwa kabla ya mfumo kuanza rasmi, na tutakapojiridhisha tutapokea na kuruhusu nauli mpya,” amesema Suluo.
Kauli hiyo imeondoa sintofahamu na minong’ono iliyokuwa imeenea mitaani kuhusu uwezekano wa kuanza kwa nauli ya shilingi 1,000 (maarufu kama nauli ya buku) katika kipindi hiki cha majaribio. LATRA imesisitiza kuwa mabadiliko yoyote ya nauli yatafanyika kwa kufuata taratibu rasmi, baada ya mapendekezo kuwasilishwa na DART na kupitia mchakato wa uthibitisho wa kisheria.
Katika kipindi hiki cha majaribio, zaidi ya mabasi 200 ya CNG (gesi asilia) yamewasili nchini, huku 37 kati yake yakiwa tayari yameanza kutoa huduma, na mengine 60 yakitumika kusaidia njia ya Kimara–Mbezi. Mfumo wa gesi katika karakana kuu za Mbagala umekamilika, hatua inayotarajiwa kupunguza gharama za mafuta na kulinda mazingira.
Wakazi wa Mbagala wameonyesha kuridhishwa na hatua hizo, wakieleza kuwa huduma hiyo imepunguza muda wa safari na kuongeza tija katika shughuli za kiuchumi.
“Tulikuwa tunapoteza muda mwingi barabarani, sasa safari ni fupi na ya uhakika,” alisema mmoja wa wakazi wa eneo hilo.
Hata hivyo, baadhi yao wameiomba LATRA na DART kuhakikisha changamoto ya upatikanaji wa kadi za usafiri inatatuliwa mapema ili wananchi wote waweze kufurahia huduma hiyo ipasavyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa UDART, Pius Ng’ingo, amesema serikali imejipanga kuhakikisha mfumo wa mwendokasi unakuwa suluhisho la kudumu kwa foleni za jiji la Dar es Salaam, huku Mkurugenzi wa MOFAT Transport Company, Abdulrahman Kassim, akitoa wito kwa wananchi kulinda miundombinu ya mradi huo kwa manufaa ya vizazi vijavyo.
Kwa ujumla, msimamo wa LATRA umeleta matumaini mapya kwa watumiaji wa usafiri huo, ukidhihirisha dhamira ya mamlaka hiyo kuendeleza usimamizi makini, unaolenga uadilifu, uwazi na kulinda maslahi ya wananchi wote.
#KhomeinTvUpdates 
✍️Mwandishi wetu
PIA USIACHE KU SUBSCRIBE
CHANEL YETU Khomein TV
YOUTUBE UWE WA KWANZA 
KUFIKIWA NA HABARI ZETU
Follow Insta & Threads @khomeintv_
Tufollow pia kwenye X (Twitter), TikTok
@khomeintv na Facebook Khomein Tv
0 Comments