RCC MTWARA YAJADAILI MIKOROSHO KUVUNWA HEWA UKAA

 

 

Baadhi ya wajumbe wa kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Mtwara (RCC) wamekuwa na mvutano juu ya miti ya Korosho kuhifadhiwa na kuingizwa kwenye biashara ya uvunaji wa hewa ukaa (Carbon Trading).

 

Mvutano wa hoja umeibuka ndani ya kikao hicho kilichofanyika leo Desemba 21, 2024 katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzaia (BoT) Tawi la Mtwara, wakati wa mjadala juu ya ziara iliyofanywa na baadhi ya viongozi, waliokwenda wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi, kujifunza masuala ya hewa ya ukaa na Chumvi.

 

Mbunge wa Viti Maalumu Anastazia Wambura alitoa pendekezo la Mikorosho kutumika kwa uvunaji wa Hewa Ukaa, kutokana na baadhi ya miti hiyo kuwa mikongwe na mingine kuachwa kwenye mapori pasipo kuhudumiwa vizuri.

 


“Kwasababu ukiangalia utaona kuna mikorosho mingi sana ambayo ipo tangu henzi za mababu, ipo na ni misitu mikubwa ambayo inaweza ikasaidia sana.” Alieleza Wambura.

 

Wazo hilo likapata upinzani kutoka kwa baadhi ya wajumbe akiwemo mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Masasi Ibrahim Chiputula, ambaye alidai kuwa misitu inayovunwa hewa ya ukaa inatakiwa isiwe na kemikali zozote, jambo ambalo ni gumu kulitekeleza kwenye mikorosho ambayo hupuliziwa dawa za kukinga wadudu kila msimu.

 


Mwenyekiti wa Tandahimba Baisa Abdallah Baisa, licha ya kukiri kuwa mikorosho inaweza kutumika kwenye biashara ya Hewa ya Ukaa, lakini akaeleza wasiwasi wake juu ya biashara hiyo huku akidai imejaa ‘ujanja ujanja’ mwingi.

 

“Haiko wazi hii biashara, hata hao Katavi wanafanya hii biashara lakini hawamjui mnunuzi na hawatokuja kumjua, Nanyumbu wameingia, Masasi wanakuja hawatokuja kumjua hata siku moja, yani ni biashara ambayo imetawaliwa na ‘middle men’ sana.” Amesema Baisa.

 


Mwenyekiti wa kikao hicho, ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Mtwara kanali Patrick Sawala, akaeleza umuhimu wa kupata maelezo ya kitaalamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira.

 

“Tunaweza tukatafuta ‘special session’ wakati tuna hiyo RCC ya wakati wa Bajeti ili tusisubiri mwishoni huko tukapata nafasi yule mtaalamu akaja hapa akatuambia..tukapata tu wajumbe tukapata elimu hiyo.” Alieleza Kanali Sawala.

 

Tayari vijiji Vinane wilayani Tanganyika vimeanza kunufaika na biashara ya hewa ukaa, ambapo takribani shilingi Bilioni 14, zinaenda kuvinufaisha vijiji hivyo.

 

#KhomeinTvUpdates

 

Juma Mohamed-Mtwara

 

PIA USIACHE KU SUBSCRIBE

CHANEL YETU Khomein TV

YOUTUBE UWE WA KWANZA 

KUFIKIWA NA HABARI ZETU

 

Follow Insta & Threads @khomeintv_

Tufollow pia kwenye X (Twitter), TikTok

@khomeintv na Facebook Khomein Tv

Post a Comment

0 Comments