MSINIPANDE KICHWANI, MSINICHUKULIE POA KISA MTOTO WA KIKE-MEYA NDILE

 

Meya wa Manispaa ya Mtwara-Mikindani, Shadida Ndile, amewaonya Madiwani na Watendaji wa Manispaa hiyo kuacha tabia ya kuchezea kiti chake kwa lengo la kumuharibia, na kudai kuwa hatokubali kuona jambo hilo likitokea.

 

Ametoa kauli hiyo leo Januari 31, 2025 katika kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya kujadili taarifa za robo ya pili ya Oktoba-Disemba.

 

Ndile, amesema “yapo mambo ambayo yanaendelea sitaki kuyaona, kama wenzangu yanawapendeza mimi hayanipendezi, hayanipendezi hata kidogo kama tumeshindwa kuheshimiana mimi nipo tayari kusimamia baraza vile nyinyi mnavyotaka. Hamuwezi mukadharau kiti, hamuwezi kiuka sheria mimi naona hilo halipo, kwahiyo kwa yeyote anayejijua yumo anayejijua siwezi nikavumilia na sina nafasi ya kuvumilia, musinipande kichwani.” Amesema Ndile na kuongeza:

 


“Kama mulikuwa mnanichukulia poa tutapelekana vile ambavyo nyinyi mnataka.”

 

Aidha, amewaonya wenyeviti wa kamati za halmashauri hiyo ambazo kimsingi zinaundwa na Meya kwa kushirikiana na Mkurugenzi, na kuwaeleza kuwa hawana mamlaka ya kumaliza kila jambo kisa wapo kwenye kamati.

 


“Mushkuru muda wenu umeisha, kuwaweka kwenye kamati sio kwamba nyie ndio watu wa kumaliza kila jambo, fanyeni kazi kwa kufuata kanuni, sheria na taratibu musinipande kichwani.

 


“Hatuna muda wa kucheza, hatuna muda wa kuchezeana na mimi sipo tayari kuchezewa, kama mulifikiria kwamba mimi mtoto wa kike mtu atanipanda kichwani dakika nilizonazo ni za kumalizia kazi ya kumsaidia Daktari Samia Suluhu Hassan, sitokuwa na aibu na sitomuogopa mtu yeyote.” Ameonya Meya Ndile.

 

Baadhi ya madiwani wa manispaa hiyo, wakizungumzia kauli hizo za Meya baada ya kumalizika kikao hicho, wakadai kuwa kauli zake ni kama ametupa jiwe gizani.

 


Diwani wa Kata ya Magomeni Lameck Mlaponi amesema “mimi kwa nafasi yangu ninamuheshimu Mheshimiwa Meya, ninatambua kwamba yeye ndio kiongozi wetu lakini na waheshimiwa madiwani wote tunaishi kwa upendo. Kwahiyo hayo kama kuna jambo lolote limetokea baya sisi binafsi hatulijui kwahiyo ni jambo la kumuuliza yeye mwenyewe au kuwauliza wenyeviti wa kamati waseme nini kinaendelea lakini sisi tunaishi kwa amani na upendo kabisa.”

 

Ahmed Kalikumbe, diwani wa kata ya Mtawanya amesema wapo baadhi ya wenyeviti wa kamati wanajifanya ‘Miungu watu’ na kumaliza kila jambo kwenye kamati zao, hivyo kuwahusisha na kalipio lililotolewa na Meya Ndile.

 

Awali akizungunza kabla ya kuahirishwa kwa Baraza hilo, Mkuu wa wilaya ya Mtwara Abdallah Mwaipaya, akaipongeza Manispaa ya Mtwara-Mikindani kwa usimamizi nzuri wa miradi ya maendeleo, huku akitoa rai kwa madiwani na watendaji kuongeza kasi ya usimamizi ili miradi inayoendelea kujengwa ikamilike kwa wakati.

 

“Wananchi wanahitaji kuona miradi ile inakamilika na kwa hakika tulishapata maelekezo kwamba kwenye miradi yote ambayo ilikuwa haijakamilika kuanzia 2021-2022, 2022-2023 mpaka 2024 ikifika Disemba mwaka jana iwe imekamilika.” Alisisitiza Mwaipaya.

 


Mwakilishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara CPA Norbert Shee, amewataka madiwani na watendaji kuondoa urasimu kwenye usimamizi wa miradi hiyo.

 

#KhomeinTvUpdates 

 

✍️ Juma Mohamed-Mtwara

 

PIA USIACHE KU SUBSCRIBE

CHANEL YETU Khomein TV

YOUTUBE UWE WA KWANZA 

KUFIKIWA NA HABARI ZETU

 

Follow Insta & Threads @khomeintv_

Tufollow pia kwenye X (Twitter), TikTok

@khomeintv na Facebook Khomein Tv

Post a Comment

0 Comments