SERIKALI YAWABANA WAKANDARASI MIRADI YA TARURA


 Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa imeagiza kufanyika tathmini ya Wakandarasi waliochelewesha miradi inayotekelezwa chini ya Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) ambayo ilipaswa kukamilika Februari 2025 ili kuwachukulia hatua ikiwamo kuwafungia wasipewe kazi popote.

Mchengerwa ametoa agizo hilo hivi karibuni  katika hafla ya utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa Soko Kuu la Majengo na vituo vya daladala jijini Dodoma kupitia mradi wa  uboreshaji miundombinu ya Miji (TACTIC) awamu ya pili unaotekelezwa chini ya Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA).

 


Amemtaka Mtendaji Mkuu wa TARURA,  Mhandisi Victor Seif na Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo kufanya tathmini hiyo na kuagiza mkandarasi anayejenga barabara za jijini Dodoma asipewe kazi kutokana na kushindwa kukamilisha ujenzi huo kwa muda uliopangwa.

 

"Haiwezekani Serikali kutoa Sh.bilioni 24 kwa ajili ya barabara, halafu watu wachache wanakwamisha jitihada za Mhe.Rais Samia. Iwe kampuni ya Kitanzania au ya kigeni, wasiwekewe tena mikataba hadi miradi yao yote iwe imekamilika," amesisitiza.

 


Pia, ameelekeza TARURA kushughulikia haraka ujenzi wa kipande cha barabara chenye urefu wa kilomita 1.8 cha Iringa Road-Michese pamoja na barabara ya mita 750 eneo la Madukani na kwamba haiwezekani Makao Makuu ya Nchi yawe na barabara za changarawe.

 


Kuhusu changamoto za kuingia na kutoka katika Kituo cha Treni cha Reli ya Kisasa (SGR) jijini Dodoma, Waziri Mchengerwa amewaagiza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mkurugenzi wa Jiji na Mkuu wa Wilaya kukaa pamoja na Shirika la Reli Tanzania (TRC) ili kuweka utaratibu mzuri wa usafiri kwa abiria.

 

Kwa upande wake, Mbunge wa Dodoma Mjini, Anthony Mavunde, amesema mradi huo utaboresha miundombinu muhimu ya Jiji hilo na kudai kuwa ujenzi wa vivuko utasaidia wanafunzi wa Mailimbili na Sechelela kuvuka makorongo wanapokwenda shule wakati wa mvua.

 

#KhomeinTvUpdates 

 

✍️Mwandishi wetu

 

PIA USIACHE KU SUBSCRIBE

CHANEL YETU Khomein TV

YOUTUBE UWE WA KWANZA 

KUFIKIWA NA HABARI ZETU

 

Follow Insta & Threads @khomeintv_

Tufollow pia kwenye X (Twitter), TikTok

@khomeintv na Facebook Khomein Tv



Post a Comment

0 Comments