SERIKALI YAFANYA MAZUNGUMZO NA TAASISI YA AEE INTEC YA AUSTRIA

 



Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt. Khatibu Kazungu imekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Teknolojia Endelevu ya Nishati (AEE INTEC) ya nchini Austria, Bw. Christopher Brunner ambaye ameeleza nia ya kampuni hiyo kuwekeza katika teknolojia mpya ya Joto la Jua (Solar thermal) inayotumika katka kuchemsha maji yanayoweza kutumika katika Shule, Hospitali, Vyuo, Viwanda na Masoko ambayo inawezesha kupunguza matumizi ya umeme.

 

Mazungumzo hayo yamefanyika jijini Gaborone nchini Botswana ambapo Dkt. Kazungu anaongoza  Ujumbe wa Tanzania kushiriki Wiki ya Nishati Endelevu kwa Nchi za Jumuiya ya Kusini mwa Afrika (SADC).

 

“Tanzania tuna rasilimali ya kutosha ya Jua ambayo inaweza kutumika kwa shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi, tunahitaji teknolojia rahisi za kisasa na za gharama nafuu katika kuendeleza Nishati ya Jua.” Amesema Kazungu

 

Katika kuhakikisha Tanzania inanufaika na programu hiyo kupitia Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) Dkt. Kazungu ameialika Taasisi ya AEE kuja nchini ili kufanya mazungumzo na Taasisi mbalimbali za Umma na Binafsi zinazohusika na uendelezaji wa nishati ya jua.

 

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya AEE, Bw. Christopher Brunner alimueleza  Dkt. Kazungu kuwa, taasisi hiyo inahusika kutoa mafunzo na kutekeleza miradi ya mifano (Solar Thermal Training & Demostration Initiative - SOLTRAIN) katika maeneo ya Nishati, Viwanda, Afya, Elimu na Kilimo kwa Afrika na duniani kwa ujumla.

 

Ameeleza kuwa kwa Afrika Taasisi hiyo inafanya kazi katika nchi mbalimbali ikiwemo Botswana, Lesotho, Afrika ya Kusini na Zimbabwe na inashirikiana na Serikali za nchi hizo katika utekelezaji wa miradi ya umeme jua kwa njia mbalimbali pamoja na kutoa mafunzo kwa wazawa kuhusu utengenezaji wa vifaa vya umeme jua.

 

Ameongeza kuwa, kampuni hiyo pia  inawajengea uwezo makundi ya vijana na wanawake katika maeneo mbalimbali yanayohusu uendelezaji wa nishati ya Jua ambapo Taasisi hiyo inatarajia kuongeza wigo wa Programu katika nchi za Malawi na Zambia.

 

 Mazungumzo kati ya Dkt. Kazungu na Bw. Brunner yalihudhuriwa na Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga na Mtaalam wa Nishati Jadidifu, Mhandisi Justine Malaba.

 

#KhomeinTvUpdates 

 

✍️ Mwandishi wetu

 

PIA USIACHE KU SUBSCRIBE

CHANEL YETU Khomein TV

YOUTUBE UWE WA KWANZA 

KUFIKIWA NA HABARI ZETU

 

Follow Insta @khomeintv_

 

Tufollow pia kwenye X (Twitter), TikTok

@khomeintv na Facebook Khomein Tv

Post a Comment

0 Comments