BODI YA ZABUNI REA YATAKIWA KUFUATA SHERIA

 

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy ameielekeza Bodi mpya ya Zabuni (Tender Board) ya Wakala kuhakikisha inatekeleza majukumu yake kwa kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu ili kuleta tija katika kazi zake. 

 

Ametoa wito huo hivi karibuni Jijini Dodoma wakati wa hafla fupi ya kuiaga Bodi ya Zabuni iliyomaliza muda wake baada ya kutumikia kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo.

 

"Ninawapongeza walioteuliwa katika Bodi mpya ya Zabuni lakini niwasisitize mhakikishe mnatekeleza majukumu yenu kwa weledi ikiwemo kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu za Ununuzi wa Umma," amesisitiza Mhandisi Saidy.

 

Aidha, ameishukuru na kuipongeza Bodi ya Zabuni iliyomaliza muda wake kwa kazi nzuri iliyofanya kipindi chote cha muda wake.

 


Amesema Bodi ya Zabuni ni chombo na nyenzo muhimu katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi na amewasihi walioteuliwa kuhakikisha wanatambua thamani waliyopewa.

 

"Bodi ya Zabuni ni muhimu sana katika uendeshaji wa shughuli mbalimbali za Ununuzi za taasisi na ukiona umeteuliwa basi elewa kuwa wewe ni mtu sahihi na hakikisha hautoki nje ya taratibu," amesisitiza Mkurugenzi Saidy.

 

Vilevile amekipongeza Kitengo cha Ununuzi kwa kazi nzuri kinayofanya na amewasisitiza kuielewa kwa undani Sheria ya Ununuzi ili kuwa na ununuzi wenye tija na uliyozingatia taratibu zote muhimu.

 

Aidha, akizungumza kwa niaba ya Bodi, Mwenyekiti wa Bodi iliyomaliza muda wake ambaye pia anaendelea kuhudumu katika Bodi mpya, Mhandisi Advera Mwijage amemshukuru Mkurugenzi Mkuu kwa ushirikiano aliotoa muda wote alipohitajika pamoja na Kitengo cha Ununuzi ambao walifanya kazi kwa karibu na Bodi.

 

"Ninawashukuru Wajumbe wa Bodi waliomaliza muda wao, tumefanya kazi kwa ushirikiano mkubwa kuhakikisha suala la Ununuzi kwa ujumla linafanyika kwa kuzingatia Sheria na miongozo iliyopo," amesema Mhandisi Advera.

 

Awali akizungumza wakati wa hafla hiyo, Katibu wa Bodi ya Zabuni REA ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi, Mapesi Manyama alifafanua Sheria zinazoelekeza uundaji wa Bodi ya Zabuni kwa taasisi.

 

"Bodi ya Zabuni inaundwa na kuendeshwa kwa mujibu wa Kifungu Namba 32 pamoja na Jedwali Namba 2 ndani ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2023 na Kanuni zake za Mwaka 2025," amefafanua Manyama. ‎

 

#KhomeinTvUpdates 

 

✍️Mwandishi wetu

 

PIA USIACHE KU SUBSCRIBE

CHANEL YETU Khomein TV

YOUTUBE UWE WA KWANZA 

KUFIKIWA NA HABARI ZETU

 

Follow Insta & Threads @khomeintv_

Tufollow pia kwenye X (Twitter), TikTok

@khomeintv na Facebook Khomein Tv

Post a Comment

0 Comments