TANZANIA KUIPA KIPAUMBELE MIKAKATI YA UTUNZAJI MAZINGIRA

 



Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango, imetoa wito kwa jamii na wadau wote wa mazingira kuendeleza juhudi zilizofanyika wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani. 

 

Juhudi hizo zinajumuisha upandaji miti, uanzishaji wa bustani za kijani na hatua madhubuti za kukemea uharibifu wa mazingira nchini. Serikali inasisitiza kuwa utunzaji wa mazingira si chaguo bali ni wajibu wa kila Mtanzania kwa ajili ya ustawi wa taifa na vizazi vijavyo.

 

Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani iliyofanyika Kitaifa katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete Juni 05,2025 Jijini Dodoma. 

 

Aidha, Makamu wa Rais amesema Serikali imeweka nia ya kupunguza athari za uharibifu wa mazingira kwa kupunguza matumizi ya nishati ya kuni na mkaa kwa shughuli za kupikia. Amesema katika kutekeleza nia hiyo, Serikali ilitoa katazo la matumizi ya kuni na mkaa kwa taasisi zinazoandaa chakula na kulisha watu zaidi ya watu mia moja kwa siku na kuzitaka zihamie katika matumizi ya nishati safi ya kupikia ambapo kufikia Machi 2025 jumla ya taasisi 762 zimeanza kutumia nishati safi ya kupikia kati ya hizo taasisi za umma ni 495 na taasisi binafsi ni 267.

 

Halikadhalika amesema jukumu la kuhamasisha na kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa hifadhi ya mazingira linahitaji ushirikiano wa wadau wote katika ngazi zote. Kupitia hilo, ametoa wito kwa vyombo vya habari, taasisi zote za Serikali, binafsi na asasi za kiraia kushirikiana katika kutoa elimu kwa jamii ili kupunguza uharibifu wa mazingira hapa nchini kwa kiasi kikubwa.

 

Vilevile amesema taarifa mbalimbali za hali ya mazingira nchini zimedhihirisha kuwepo kwa uharibifu wa ardhi katika maeneo mbalimbali nchini, ambapo inakadiriwa kuwa takriban asilimia 61 ya ardhi nchini iko katika hatari ya kuharibika. Amesema uharibifu huo unachangiwa kwa kiasi kikubwa na shughuli za kibinadamu zisizo endelevu, idadi kubwa ya mifugo isiyolingana na uwezo wa malisho, ukataji wa misitu kwa ajili ya kuni na mkaa, uanzishaji wa mashamba mapya unaotokana na kilimo cha kuhamahama, uchimbaji holela wa madini pamoja na upanuzi wa makazi usiozingatia mipango miji.

 

Naye Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Khamis Hamza Khamis amewahimiza wadau wa mazingira na jamii kwa ujumla, kuanza na mabadiliko tabiawatu ili kuweza kudhibiti mabadiliko tabianchi kupitia kuhamasisha matumizi ya teknolojia za urejelezaji wa taka ozo na za plastiki, kupunguza ukataji miti holela kwa ajili ya kuni na mkaa na kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia.

 

Amesisitiza kuwa, katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira, Serikali imechukua hatua mbalimbali za kisera na kimkakati ikiwa ni pamoja na kupitishwa kwa Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021, Mpango Kabambe wa Taifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (2022-2032), kuongeza kasi ya upimaji wa ardhi na umilikishaji wa ardhi kimila.

 

Hatua nyingine ni pamoja na uhamasishaji wa matumizi endelevu ya ardhi hususan kilimo mseto, kilimo cha matuta, kilimo hifadhi na mbinu endelevu za kiasili za hifadhi ya malisho. na utekelezaji wa hatua hizi ikiwa ni pamoja na kuendelea kuhamasisha utunzaji wa mazingira kwa ujumla.

 

#KhomeinTvUpdates 

 

✍️Mwandishi wetu

 

PIA USIACHE KU SUBSCRIBE

CHANEL YETU Khomein TV

YOUTUBE UWE WA KWANZA 

KUFIKIWA NA HABARI ZETU

 

Follow Insta & Threads @khomeintv_

Tufollow pia kwenye X (Twitter), TikTok

@khomeintv na Facebook Khomein Tv

Post a Comment

0 Comments