TANZANIA NA SOMALIA ZAIMARISHA USHIRIKIANO WA KIDIPLOMASIA

 


Katika kile kinachoonekana kuwa hatua nzuri ya kuimarisha ushirikiano wa kihistoria na kidiplomasia kati ya Tanzania na Somalia, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Shirikisho la Somalia,  Abdisalam Abdi Ali, Juni 29,2025 amewasili nchini kwa ziara ya kikazi yenye umuhimu wa kipekee.

 

Abdisalam amepokelewa kwa heshima katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa. Ujio wa Waziri huyo unaakisi uhusiano imara uliopo kati ya Mataifa haya mawili ya Pembe na Mashariki mwa Afrika.

 

Aidha, Waziri Abdisalam yupo nchini kuhudhuria Maadhimisho ya Miaka 65 ya Uhuru wa Somalia, tukio ambalo linabeba uzito mkubwa wa kihistoria kwa Taifa lake. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,  Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika sherehe hizo, hii ni ishara ya heshima na mshikamano wa dhati baina ya nchi hizi mbili.

 

Lakini zaidi ya maadhimisho, ziara hii inalenga kuendeleza mazungumzo ya kina ya ushirikiano wa pande mbili, ambapo viongozi hao watajadili fursa mpya za kushirikiana katika maeneo muhimu kama:

Diplomasia ya kiuchumi na uwekezaji, Elimu na mafunzo ya kijeshi na kidiplomasia, Usalama wa kikanda na amani ya mipaka,

 

Pamoja na kubadilishana utaalamu wa maendeleo na teknolojia, Utalii, utamaduni na michezo ambapo,

Katika kuthibitisha dhamira ya ushirikiano wa kiutalii, Waziri Abdisalam pia anatarajiwa kutembelea Mbuga ya Wanyama ya Mikumi mkoani Morogoro kivutio maarufu cha urithi wa asili wa Tanzania. 

 

Ziara hiyo inalenga kufungua njia ya kuvutia watalii kutoka Somalia, kuendeleza diplomasia ya utalii na kuimarisha uchumi wa kijani.

 

Tanzania na Somalia zimekuwa marafiki wa muda mrefu, zikiwa zimeunganishwa na misingi ya harakati za ukombozi, mshikamano wa kidugu, na malengo ya pamoja ya Afrika yenye amani, maendeleo na mshikamano. Kupitia mikutano ya kidiplomasia kama hii, Mataifa hayo yanajenga daraja la maelewano, biashara na maendeleo jumuishi kwa manufaa ya wananchi wao.

 

Ziara hii ya Waziri Abdisalam Abdi Ali ni ujumbe wenye nguvu unaoonyesha dhamira ya pamoja ya Tanzania na Somalia kuandika sura mpya ya ushirikiano wa kimkakati. Ni mwanzo wa ukurasa wa matumaini, mshikamano na ustawi wa pamoja katika Afrika Mashariki.

 

#KhomeinTvUpdates 

 

✍️Mwandishi wetu

 

PIA USIACHE KU SUBSCRIBE

CHANEL YETU Khomein TV

YOUTUBE UWE WA KWANZA 

KUFIKIWA NA HABARI ZETU

 

Follow Insta & Threads @khomeintv_

Tufollow pia kwenye X (Twitter), TikTok

@khomeintv na Facebook Khomein Tv


Post a Comment

0 Comments