WATENDAJI UCHAGUZI TOENI TAARIFA KWA VYAMA VYA SIASA - JAJI MWAMBEGELE

 

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kupitia Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jacobs Mwambegele imewataka watendaji wa Uchaguzi Mkuu  2025 kutoa taarifa mapema kwa vyama vya siasa kuhusu utaratibu wa kuwaapisha Mawakala.

 

Mwambegele ameyasema hayo mkoani Shinyanga Julai 21, 2025 wakati akifungua mafunzo kwa watendaji wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2025.

 

“Wakati wa kuapisha mawakala, toeni taarifa mapema kwa vyama vya siasa kwa mujibu wa sheria, kanuni na maelekezo ya Tume na kuvipatia vyama vya siasa orodha ya vituo vya kupigia kura ili kuviwezesha kupanga mawakala,” amesema Jaji Mwambegele. 

 

Pia amewasisitiza watendaji hao kuhakikisha vifaa vya uchaguzi wanavyopokea kutoka Tume, wanavihakiki, kuvikagua na kuhakikisha vinasambazwa kwenye vituo vyote na kila mkuu wa kituo anapata vifaa vyote vya uchaguzi vinavyohitajika mapema.

 

Aidha amewataka kuhakikisha kuwa,wanaweka utaratibu siku ya uchaguzi, utakaowezesha kila kituo cha kupigia kura kufunguliwa saa 1:00 kamili asubuhi na kufanya mawasiliano na Tume pale ambapo ushauri utahitajika kuhusiana na masuala ya uchaguzi.

 

Naye Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Rufani (Mstaafu) Mbarouk Salim Mbarouk wakati akifungua mafunzo hayo, amewaasa watendaji hao kufanya kazi kwa kuzingatia Katiba, Sheria, Kanuni, miongozo na maelekezo mbalimbali yaliyotolewa na yatakayotolewa na Tume.

 

 “Jitahidini na mjiepushe kuwa vyanzo vya malalamiko kutoka kwa vyama vya siasa na wadau wa uchaguzi. Hakikisheni mnazingatia ipasavyo Katiba, Sheria, Kanuni, Miongozo na maelekezo mbalimbali yaliyotolewa na yatakayotolewa na Tume,” amesema Jaji Mbarouk.

 

Amesisitiza ushirikishwaji wa wadau wa uchaguzi kwenye maeneo wanayopaswa kushirikishwa kwa mujibu wa Katiba, Sheria, Kanuni, miongozo na maelekezo ya Tume.

 

Amewakumbusha kuhusu wajibu wao wa kuhakikisha wanavitambua vituo vya kupigia kura mapema ili kubaini mahitaji maalum ya vituo husika na kuhakikisha kunakuwa na mpangilio mzuri ambao utaruhusu uchaguzi kufanyika kwa utulivu na amani.

 

“Ajira za watendaji wa vituo zizingatie kuajiri watendaji wenye weledi, wanaojitambua, wazalendo, waadilifu na wachapakazi na kuachana na upendeleo kwa ndugu na jamaa ambao hawana sifa za kufanya shughuli za uchaguzi,” amesema Jaji Mbarouk.

 

Mafunzo hayo yanafanyika kwa siku tatu kwenye mikoa mbalimbali nchini kwa siku tatu na yanawajumuisha waratibu wa uchaguzi, wasimamizi wa uchaguzi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo.

 

Tume imeyagawa mafunzo hayo kwenye awamu mbili ambapo awamu hii ya pili inahusisha mikoa ya Simiyu, Shinyanga, Kusini Pemba, Kaskazini Pemba, Mwanza, Mara, Dar es Salaam, Pwani, Rukwa, Katavi, Manyara, Arusha, Songwe na Mbeya. 

 

Ambapo awamu ya kwanza imefanyika Julai 15 hadi 17, 2025 na ilihusisha watendaji kutoka mikoa ya Morogoro, Singida, Dodoma, Kaskazini Unguja, Kusini Unguja, Mjini Magharibi, Geita, Kagera, Mtwara, Lindi, Tabora, Kigoma, Tanga, Kilimanjaro, Ruvuma, Iringa na Njombe.

 

#KhomeinTvUpdates 

 

✍️Mwandishi wetu

 

PIA USIACHE KU SUBSCRIBE

CHANEL YETU Khomein TV

YOUTUBE UWE WA KWANZA 

KUFIKIWA NA HABARI ZETU

 

Follow Insta & Threads @khomeintv_

Tufollow pia kwenye X (Twitter), TikTok

@khomeintv na Facebook Khomein Tv

Post a Comment

0 Comments