TUME YATOA KIBALI KWA ASASI ZA KIRAIA 256

 

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetoa vibali vya kutoa Elimu ya Mpiga Kura wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kwa taasisi na asasi za kiraia 164 na kibali cha uangalizi wa uchaguzi kwa taasisi na asasi 76 za ndani ya nchi na 12 za Kimataifa.

 

Taarifa ya Tume kwa vyombo vya habari iliyotolewa Julai 19, 2025 na kusainiwa na Mkurugenzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) Ramadhani Kailima imesema Tume imefikia uamuzi wa kutoa vibali hivyo katika kikao chake kilichoketi Julai 18, mwaka huu.

 

“Kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 10(1) (g) (h) cha Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya mwaka 2024 kikisomwa pamoja na Kanuni ya 22 ya Kanuni za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi za mwaka 2024, katika kikao chake maalum kilichofanyika Julai 18, 2025 Tume imeridhia na kutoa kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kwa taasisi na asasi za kiraia 164.,”amesema Kailima katika taarifa hiyo.

 

 Aidha, Kailima amesema katika kikao hicho kuwa, Tume imeridhia na kutoa kibali cha uangalizi wa uchaguzi kwa taasisi na asasi 76 za ndani ya nchi na 12 za Kimataifa. 

 

Taarifa hiyo ya Kailima imesema Tume imefanya uamuzi huo kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 10(1)(i) cha Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya mwaka 2024 kikisomwa pamoja na kifungu cha 85(4) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Na. 1 ya Mwaka 2024 na kanuni ya 13(1) na (2) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za Mwaka 2025.

 

Orodha ya taasisi na asasi husika inapatikana kupitia tovuti ya Tume ya www.inec.go.tz na mitandao ya kijamii ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.

 

“Taasisi na asasi za kiraia zilizoridhiwa na kupewa kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura zitajulishwa kwa njia ya barua pepe kupitia Mfumo wa Usajili (Accreditation Management System) ili kujaza taarifa za kuwawezesha kukamilisha taratibu nyingine ikiwemo kuweka orodha ya watu watakaotoa elimu hiyo,”imesema sehemu ya taarifa hiyo ya Tume. 

 

Aidha, Kwa upande wa taasisi na asasi za kiraia zilizopata kibali cha kuwa waangalizi wa uchaguzi zimetakiwa kuwasilisha kwa njia ya Mfumo wa Usajili (Accreditation Management System) majina ya waangalizi na maeneo waliyopangiwa kufanya uangalizi huo kwa ajili ya kuwaandalia vibali.

 

Tume imebainisha kuwa, taarifa zingine zote muhimu kuhusu utekelezaji wa majukumu ya utoaji wa elimu ya mpiga kura na uangalizi wa uchaguzi, miongozo na taratibu zote zitatolewa mapema iwezekanavyo.

 

Tume imezipongeza taasisi na asasi za kiraia ambazo zimepata kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura na kuwa waangalizi wa Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2025.

 

#KhomeinTvUpdates 

 

✍️Mwandishi wetu

 

PIA USIACHE KU SUBSCRIBE

CHANEL YETU Khomein TV

YOUTUBE UWE WA KWANZA 

KUFIKIWA NA HABARI ZETU

 

Follow Insta & Threads @khomeintv_

Tufollow pia kwenye X (Twitter), TikTok

@khomeintv na Facebook Khomein Tv

Post a Comment

0 Comments