SERIKALI YA RAIS SAMIA KUSOGEZA HUDUMA ZA KIJAMII HANANG

 

Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa imesema itajenga shule, zahanati, sekondari na kituo cha afya ili kusogeza huduma za kijamii kwenye makazi mapya ya waathirika wa maporomoko ya tope Hanang mkoani Manyara.

 

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amesema hayo hivi karibuni akiwa Wilayani Hanang, wakati akikabidhi nyumba 109 kwa waathirika wa maporomoko ya tope wilayani humo, ambazo zimejengwa na Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Msalaba Mwekundu kwenye Kitogoji cha Waret kijiji cha Gidagamowd.

 

“Tunataka wananchi hawa wawe na mwingiliano na wengine, waendelee kuishi hapa na wapate huduma muhimu za kijamii na ndio maana tutajenga shule, zahanati, sekondari na kituo cha afya,” Mhe. Majaliwa amesisitiza.

 

Aidha, amefafanua kuwa, kati ya nyumba 109 alizozikabidhi kwa waathirika wa maporomoko ya tope, nyumba 73 zimegharamiwa na Serikali, nyumba 35 zimegharamiwa na Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania na nyumba moja imegharamiwa na Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT).

 

Ameongeza kuwa, nyumba zote hizo zimejengwa kwa uratibu mzuri wa timu ya wataalam kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Fedha, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Hanang pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Hanang.

 

Waziri Mkuu ameipongeza na kuishukuru TARURA kwa ujenzi mzuri wa barabara kwenye eneo hilo ambalo zimejengwa nyumba 109 za waathirika wa maporomoko ya tope na kuongeza kuwa toka amefika na kuanza ukaguzi wa nyumba hajaona barabara iliyoteleza licha uwepo wa mvua iliyokuwa ikinyesha.

 

“Waziri wa TAMISEMI na TARURA yako mmefanya kazi nzuri sana ya ujenzi wa barabara kwenye nyumba hizi 109, hivyo jukumu mlilobakia nalo ni kutuwekea lami hivyo jaribu kuangalia kwenye vifungu vyako vya bajeti ili barabara ziwekwe lami."  

 

Maporomoko ya tope wilayani Hanang yaliyotokea DIsemba 7, 2023 katika mji mdogo wa Katesh pamoja na vijiji jirani yalisababisha baadhi ya wakazi wa maeneo hayo kupoteza nyumba za kuishi, hivyo Serikali ilichukua hatua ya kukabiliana na changamoto hiyo na hatimaye Waziri Mkuu  amekabidhi nyumba 109 kwa waathirika wa maporomoko hayo.

 

#KhomeinTvUpdates 

 

️Mwandishi wetu

 

PIA USIACHE KU SUBSCRIBE

CHANEL YETU Khomein TV

YOUTUBE UWE WA KWANZA 

KUFIKIWA NA HABARI ZETU

 

Follow Insta & Threads @khomeintv_

Tufollow pia kwenye X (Twitter), TikTok

@khomeintv na Facebook Khomein Tv

Post a Comment

0 Comments