Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya Uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, kwa kuthamini wananchi wake, imeahidi kuendelea kukusanya Kodi bila ya kutumia mabavu, na watazidi kutumia utaratibu wa kutoa elimu na kuwasikiliza walipa kodi, kwa kuwafuata katika maeneo yao.
Uamuzi huu unatokana na busara za Rais wa Awamu ya Sita Dkt. Samia ambae amefanya jitihada katika kuondoa malalamiko kwa wananchi kuhusiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kukusanya kodi kwa kutumia nguvu.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw.Yusuph Mwenda amesema, Mamlaka hiyo imebadilisha utaratibu wa ukusanyaji kodi kutoka kwa walipakodi na badala yake watatumia utaratibu wa kutoa elimu kwa walipakodi.
Akiwa Jijini Arusha alikokwenda kwa lengo la kuwashukuru na kuwasikiliza walipakodi, Kamishna Mkuu Mwenda ameahidi kuendelea kushirikiana na walipakodi Mkoani humo na kuainisha kuwa, katika mwezi Disemba, Mameneja watawafuata walipakodi na kuwashukuru huku wakisikiliza changamoto zao na kuzitatua.
Akizungumza na mmoja wa wafanyabiashara wanaounda magari ya kubebea Watalii Jijini Arusha Kamishna Mkuu Mwenda amesema, TRA inatambua mchango mkubwa unaotolewa na wafanyabiashara pamoja na Wawekezaji katika maendeleo ya Taifa kupitia kodi wanazolipa.
Amesema kwa kutambua thamani ya walipakodi ameamua kuwafuata na kuwashukuru ili kuwapa motisha ya kuendelea kulipa kodi kwa ustawi wa maendeleo ya nchi.
Hatua hii ya kuwafuata walipa kodi na kuwasikiliza changamoto zao inaboresha mazingira ya walipa kodi hao na kuwatambulisha kuwa wao na TRA siyo maadui bali ni watu wanaojenga nyumba moja.
Akiwa katika Ofisi za World Vision Tanzania Mkoani Arusha, Kamishna Mkuu Mwenda amesema Shirika hilo lisilokuwa la kiserikali lililoajiri wafanyakazi takribani 500 wamekuwa ni walipakodi wazuri wasiokuwa na udanganyifu katika kodi na wanaozingatia sheria.
Amesema, yapo mashirika yasiyo ya kiserikali yanayofanya kazi za kijamii yanayofanana na World Vision lakini yamekuwa siyo walipa kodi wazuri na kuwataka kuiga mfano wa World Vision katika kulipa kodi, ambapo World Vision inafanya kazi katika Mikoa 15, na kuwataka waangalie uwezekano wa kwenda Mikoa mingine mpaka Visiwani Zanzibar, kwa kuwa wamekuwa na msaada mkubwa kwa jamii hasa watoto waliopo katika mazingira hatarishi na jamii zisizokuwa na uwezo.
Amewaambia World Vision, milango ipo wazi kwao kufanya mazungumzo na TRA kuhusu masuala ya kikodi waliyoomba kusaidiwa na mazungumzo hayo yatafanywa kwa kufuata sheria ili kuweka usawa kwa kila upande.
Kamishna Mkuu Mwenda pia ametembelea kampuni ya Enza Zaden Africa inayomiliki mashamba ya kuzalisha mbegu na kujionea uendeshaji wa shughuli zao huku akiwapongeza kwa kukua na walipakodi wa kati na waaminifu katika ulipaji kodi.
#KhomeinTvUpdates
✍️Mwandishi wetu
PIA USIACHE KU SUBSCRIBE
CHANEL YETU Khomein TV
YOUTUBE UWE WA KWANZA
KUFIKIWA NA HABARI ZETU
Follow Insta & Threads @khomeintv_
Tufollow pia kwenye X (Twitter), TikTok
@khomeintv na Facebook Khomein Tv
0 Comments