Wafanyabiashara na wadau mbalimbali wa Biashara Mkoa wa Mtwara, wamefanya kikao kilicholenga kutoa Maoni, Kero, Changamoto na Mapendekezo kwa Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi.
Kikao hicho kimefanyika Mjini Mtwara leo Januari 31, 2025 na kuongozwa na Kaimu Mwenyekiti wa Tume hiyo Mwanaidi Sinare Majaar ambaye ameeleza kuwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan aliunda Tume hiyo ambayo inazunguka nchi nzima ili kupata maoni ya wafanyabiashara katika kero zinazowakabili ikiwemo utitiri wa Kodi.
"Utitiri wa Kodi katika biashara ndio ulimfanya Mhe.Rais Dkt.Samia kuunda Tume ya kutazama mifumo mbalimbali ya Kodi na kuweza kutoa mapendekezo ya kufanya maboresho ya kuhakikisha kuwa kodi inakusanywa lakini pia kuondoa mzigo kwa walipakodi" ameeleza Kaimu Mwenyekiti.
Akifungua Kikao hicho Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara Abdillah Mfinanga, alisema kuwa ujio wa Tume hiyo ni fursa kwa wafanyabiashara katika mkoa huo kutoa maoni, kero, changamoto na mapendekezo ya maboresho ya Kodi.
Akitoa maoni katika kikao hicho, Mwenyekiti Chemba ya wafanyabiashara Wanawake Tanzania Mkoa wa Mtwara Bi.Mwajuma Ankoni ameipongeza Tume hiyo ambayo amesema itasaidi kusikiliza kero za wafanyabiashara na kuzipeleka kwa Mhe.Rais kwa ajili ya utatuzi.
Naye Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Soko Kuu la Mtwara Mshamu Said Kaisi, ameshauri juu ya kushusha viwango vya kodi kwa bidhaa zinazotoka nchi jirani ya Msumbiji ili kuvutia wafanyabishara wengi zaidi na kuchangamsha uchumi wa Mkoa.
Aidha, kwa upande wake Mtumba said Hashimu, katibu Soko Kuu Mtwara ameshauri juu ya uanzishwaji wa mitaala ya kufundishia shuleni itakayokuwa inahusu masuala ya Kodi, ili kutengeneza kizazi kitakachokuwa na uelewa wa mambo ya Kodi ambayo hivi sasa kuna baadhi ya watu wanayaona kuwa ni kero kwao.
✍️ Bryson Mshana-Mtwara
PIA USIACHE KU SUBSCRIBE
CHANEL YETU Khomein TV
YOUTUBE UWE WA KWANZA
KUFIKIWA NA HABARI ZETU
Follow Insta & Threads @khomeintv_
Tufollow pia kwenye X (Twitter), TikTok
@khomeintv na Facebook Khomein Tv
0 Comments