Mteule wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tamisemi anayeshughulikia Miundombinu Mhandisi Rogatus Mativila ameagiza wakandarasi wanaojenga barabara za Engosheraton, Olasiti na Oljoro patakapojengwa stendi mpya ya mabasi kwa Jiji la Arusha zikamilike kwa wakati.
Agizo hilo limetolewa Jijini humo na Mhandisi Mativila wakati alipotembelea barabara hizo tatu zenye urefu wa kilomita 12.1 kupitia Mradi wa Kuboresha Miji (TACTIC) uliopo chini ya TARURA.
Amesema barabara hizo tatu za Engosheraton, Olasiti na Oljoro zenye thamani ya shilingi bilioni 15.4 zinajengwa kwa kiwango cha lami lakini bado ukamilishwaji wake upo nje ya muda.
Akizungumza mara baada ya kutembelea barabara hizo Mhandisi Mativila amesema ziara hiyo ni ya kawaida katika kuangalia maendeleo ya kazi zinazofanywa katika ujenzi wa barabara hizo.
“Ujenzi wa barabara ya Oljoro bado upo nyuma kwa asilimia 35 kutokana na kubadilishwa kwa mchoro(dizaini) kutokana na kiwango chake cha usanifu na kuwa barabara ya Mkoa kutokana na ujenzi wa stendi mpya ya mabasi”.
“lakini pia barabara hii itakuwa ni kiunganishi cha barabara kuu inayoenda hadi Dodoma hapo baadaye”Ameongeza Mhandisi Mativila.
Hata hivyo amesema tathimini ya kuongeza muda wa ujenzi wa barabara hiyo ya Oljoro imeshafanyika kwa sababu mradi huo ulipaswa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu.
"Tulipaswa kuwa asilimia 99 katika mradi huu na sasa wakandarasi wanatakiwa kukamilisha mradi huo Juni mwaka huu huku mvua zikitegemea kunyesha muda wowote hivyo lazima wakamilishe barabara hizi"
Pia amesisitiza mradi huo wa barabara hizo tatu kukamilika kwa haraka ili Juni mwaka huu, zikabidhiwe na kusisitiza ubora ni jambo la msingi sana.
"Sijaridhika na hatua hii lakini kuna changamoto zilijitokeza hivyo wazirekebishe kwani serikali inatumia fedha nyingi katika shughuli za maendeleo hivyo lazima wasimamizi na wajenzi wa barabara hizi wakamilishe kwa wakati.
Naye, Msimamizi wa mradi huo kutoka kampuni ya ujenzi ya Mhandisi Consultant Ltd ,Mhandisi John Benedict amesema kama wahandisi wanashukuru kwa serikali kukubali changamoto hizo huku akiahidi kwamba mradi huo utakamilika Juni mwaka huu.
Aidha, amesema wataongeza timu ya kazi ili kupima maendeleo ya mradi anaojenga mkandarasi huyo ili kufikia malengo kwani mradi huo unatembelewa mara kwa mara na mkandarasi analipwa kwa wakati.
Awali Mhandisi Sofa Edward kutoka Jiji la Arusha ambao wao ndio wasimamizi wakuu aliahidi kusimamia wakandarasi hao ili wamalize kwa wakati kazi hiyo kwani wananchi wa kata hizo wanazihitaji kwa ajili ya kurahisisha usafiri ikiwemo wananchi kupata maendeleo.
✍️Mwandishi wetu
PIA USIACHE KU SUBSCRIBE
CHANEL YETU Khomein TV
YOUTUBE UWE WA KWANZA
KUFIKIWA NA HABARI ZETU
Follow Insta & Threads @khomeintv_
Tufollow pia kwenye X (Twitter), TikTok
@khomeintv na Facebook Khomein Tv
0 Comments