Serikali ya awamu ya Sita inayongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Kaimu Mkurugenzi huduma za Tiba kutoka Wizara ya Afya ambaye pia ni Mkurugenzi Msaidizi huduma za Kinywa na Meno Dkt. Baraka Nzobo imetoa wito kwa wakurugenzi, wasimamizi na viongozi wa makundi mbalimbali kujenga utamaduni wa kuwatembelea watoa huduma katika vituo na maeneo yao ya kazi, ili kuwaongezea morali ya ufanyaji kazi.
Dkt. Nzobo ametoa rai hiyo Februari 5, 2025 wakati wa zoezi la usimamizi shirikishi katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa Makiungu na Zahanati ya Dung’unyi wilayani Ikungi, mkoani Singida.
"Utekelezaji wa zoezi hili utasaidia watoa maamuzi kujua changamoto zilizopo maeneo ya kazi na vituoni hususani vijijini, nje ya miji na kwa watumishi na watoa huduma, jambo litakalosaidia kwenye uandaaji wa mipango ya bajeti na bajeti kwa ujumla kuwa na uhalisia" amesema Dkt. Nzoba na kuongeza.
“Ofisini tunakaa tunafanya kazi, lakini unapotoka kwenda kuwatembelea watoa huduma na watumishi kwenye vituo inaleta mwamko na ari ya ufanyaji kazi, lakini pia kuona hali halisi ya changamoto ambazo watumishi wanakutana nazo wakati wa utekelezaji wa majuku yao" amesisitiza Dkt. Nzobo.
Dkt. Nzobo amesema usimamizi shirikishi unasaidia kujengeana uwezo, kutatua changamoto zinazowakabili watoa huduma na kuboresha hali ya ubora wa huduma kama inavyosisitizwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akitoa taarifa ya Hospitali Mkurugenzi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Makiungu Dkt. Alesandro Nava ameainisha malengo ya hospitali hiyo kuwa ni kusogeza karibu huduma za afya za msingi na za kibingwa kwa watu wote na hasa watu wa mazingira ya kawaida na wa kipato cha chini, malengo ambayo hutekelezwa kwa kuandaa miundombinu ya afya, kutoa huduma bora za afya kwa gharama za chini, kipaumbele kikitolewa kwa huduma za mama na mtoto.
Mkurugenzi huyo pia ameishukuru Serikali kwa ushirikiano ambao umeiwezesha kutoa fungu toka MSD kwa ajili ya dawa na vifaa tiba, gari la wagonjwa, pia kati ya watumishi 362 watumishi 81 wanalipwa na Serikali, jambo ambalo linaisaidia hospitali kutoa huduma kwa ufanisi na ufasaha.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Dung’unyi iliyopo kijiji cha Munkinya wilaya ya Ikungi Bi. Advera Patrick amesema Zahanati inahudumia wananchi wapatao 13,191 kutoka vijiji vitano (5) vya Dung'unyi, Samaka, Damankia, Munkinya na Kipumbuiko.
“Kwa kipindi cha Julai 2024 hadi Januari 2025 jumla ya waliojifungua ni 215, watoto waliopata chanjo ni 1,694 kati ya hao watoto 940 walipata huduma kituoni na watoto 754 walipata chanjo kupitia huduma za kliniki mkoba, huku
jumla ya akina mama wajawazito waliopata huduma za kliniki ni 1,939, kati ya hao wajawazito 1,159 walipata huduma kituoni na wajawazito 780 walipata huduma za mkoba, huku hali ya upatikanaji wa dawa muhimu na vifaa Tiba Kituoni ikiwa ni asilimia 98,” amesema Bi. Adveria.
✍️Mwandishi wetu
PIA USIACHE KU SUBSCRIBE
CHANEL YETU Khomein TV
YOUTUBE UWE WA KWANZA
KUFIKIWA NA HABARI ZETU
Follow Insta & Threads @khomeintv_
Tufollow pia kwenye X (Twitter), TikTok
@khomeintv na Facebook Khomein Tv
0 Comments