TUSIONE UZEE KAMA NI UCHAWI, TUWATUNZE WAZEE WETU-GWAKISA

 



Wazee wapatao 204 ndani ya Manispaa ya Mtwara-Mikindani, wamepatiwa kadi za Bima ya Afya ya Jamii (ICHF) iliyoboreshwa, kutoka kwa taasisi ya Nanauka Foundation, zitakazowasaidia kupata matibabu kwa muda wa mwaka mmoja.

 


Akizungumza kwenye hafla hiyo leo Februari 28, 2025, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara-Mikindani Gwakisa Mwasyeba, amesisitiza jamii kuendelea kuwatunza wazee na kuachana na dhana ya kuwahusisha na ushirikina.

 


“tusione wazee kama ni uchawi, unajua wengine wanaweza kutaka kurithi vitu kwa babaake, mimi naamini tafuta cha kwako, kile alichotafuta mzee ni cha kwake na mke wake, yani mali yake kwahiyo akiamua kukupa wewe apende, sasa maeneo mengine utakuta wanaanza kuwaua wazee wetu, wakati maeneo mengine sisi tunawahitaji wazee wetu.” Amesisitiza Mwasyeba.

 


Mkurugenzi wa taasisi hiyo Joel Nanauka, akizungumza baada ya zoezi hilo, amesema walipokea maombi kutoka kwa Baraza la Wazee la Mkoa wa Mtwara juu ya uhitaji wa kadi za matibabu.

 


“Walituomba tuweze kudhamini matibabu yao kwa kuwapatia bima ya afya ya mwaka mmoja, sisi baada ya kupokea ombi lile tukaona ni jambo kubwa la muhimu kulifanya kwa kuzingatia kwamba wapo wazee ambao hawajabahatika kuwa na pensheni pengine, au wengine hawana watoto kwamfano wa kuweza kuwapatia hayo matibabu kwahiyo kama jukumu letu la kawaida katika jamii tukaona ni jambo linalofaa sana kuwasaidia.” Amesema Joel.

 


Diwani wa kata ya Chuno, Fanikio Chijinga, akapongeza juhudi za taasisi ya Nanauka Foundation kwa kuwasaidia wazee, huku akikiri kuwa inawapunguzia mzigo viongozi katika kuwahudumia watu wenye makundi maalumu.

 


Baadhi ya wazee waliokabidhiwa bima hizo, wakaomba serikali kuajili madaktari wazee kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.

 

“Kuna tiba zingine hazitakiwi za kitaalamu, kuna tiba zingine zinatakiwa yule mzee aliyekaa pale dokta atamwambia mzee mwenziye bwana wee..nenda kachume majani kadha, kadha, kadha weka jikoni jifinyangefinyange utakuwa tayari umeshatibiwa, ni maarifa kutoka kwa nani! Kwa dokta mzee.” Amesema mzee Seleman Kombo.

 


Kwa mujibu wa matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, mkoa wa Mtwara unashika nafasi ya pili Kitaifa kuwa na idadi kubwa ya wazee wenye umri wa kuanzia miaka 60 na kuendelea, ukiwa na asilimia 9.1, baada ya mkoa wa Kilimanjaro unaoshika nafasi ya kwanza kwa asilimia 10.4.

 

Hii ni awamu ya pili kwa taasisi ya Nanauka Foundation kugawa kadi za matibabu kwa wazee, ambapo awamu yakwanza iligawa kwa Wajane 100.

 

#KhomeinTvUpdates 

 

✍️ Juma Mohamed-Mtwara

 

PIA USIACHE KU SUBSCRIBE

CHANEL YETU Khomein TV

YOUTUBE UWE WA KWANZA 

KUFIKIWA NA HABARI ZETU

 

Follow Insta @khomeintv_

 

Tufollow pia kwenye X (Twitter), TikTok

@khomeintv na Facebook Khomein Tv

Post a Comment

0 Comments