Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Abdallah Mwaipaya, amewataka watumishi wa Umma wote wilayani humo na kanda ya kusini kwa ujumla, kufuata matakwa ya kisheria kwenye kufanya manunuzi ya umma kwa kutumia mfumo wa NeST.
Mwaipaya, ametoa maelekezo hayo Februari 28, 2025 mjini Mtwara wakati akifungua semina ya wanahabari wa mkoa wa Mtwara, iliyoandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), iliyolenga kuwajengea uwezo wa kufahamu taratibu za manunuzi ya umma.
“Kila mtumishi ahakikishe anazingatia matakwa ya sheria kwa kutumia mfumo wa NeST kufanya ununuzi wa umma wa jambo lolote linalohusu manunuzi ya umma, kama unahitaji ufafanuzi au kama una changamoto sasa ofisi za PPRA zipo karibu na wewe na unaweza kuwafikia kwa njia nyingine ya simu na kadhalika.” Amesema Mwaipaya.
Aidha, Mwaipaya baada ya ufunguzi wa semina hiyo, akaongoza zoezi la uzinduzi wa ofisi za PPRA Kanda ya kusini zilizopo kwenye jengo la Sokoine, mjini Mtwara.
Kwa upande wake, meneja wa PPRA Kanda ya kusini Finias Manase, akaeleza fursa ambazo wananchi wanaweza kunufaika nazo kupitia mfumo wa NeST, akisema “kama wananchi wakijua hizi fursa na wakashiriki inavyostahili ni kwamba watapata tuzo za mikataba, na watakwenda kufaidi hii asilimia 70 ya keki ya taifa ambayo ipo kwenye eneo la ununuzi.”
Kupitia mfumo wa NeST, wananchi wanaweza kuomba tenda zinazotangazwa na serikali, iwapo watakidhi vigezo vinavyotakiwa ikiwa ni pamoja na kusajili vikundi au kampuni kulingana na miongozo inavyoelekeza.
Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mtwara (MTPC) Grace Kasembe, akawashukuru PPRA kwa kuona umuhimu wa kukutana na waandishi wa habari wa mkoa kuwapa elimu juu ya mfumo wa ununuzi wa umma.
#KhomeinTvUpdates
✍️ Juma Mohamed-Mtwara
PIA USIACHE KU SUBSCRIBE
CHANEL YETU Khomein TV
YOUTUBE UWE WA KWANZA
KUFIKIWA NA HABARI ZETU
Follow Insta @khomeintv_
Tufollow pia kwenye X (Twitter), TikTok
@khomeintv na Facebook Khomein Tv
0 Comments