Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA) imewataka watoa huduma za tiketi mtandaoni kuhakikisha mifumo yao imeunganishwa na mifumo ya serikali inayosimamiwa na LATRA pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ifikapo tarehe 1 Julai 2025.
Agizo hilo ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha usimamizi wa sekta ya usafiri ardhini, kuongeza uwazi katika ukusanyaji wa mapato, na kuhakikisha abiria wanapata huduma kwa mujibu wa sheria na viwango vinavyokubalika.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Morogoro wakati wa ukaguzi wa utekelezaji wa masharti ya leseni za usafirishaji abiria, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa LATRA, Salum Pazzy, amesema ni wachache tu kati ya watoa huduma 15 waliokamilisha usajili na kuunganisha mifumo yao na ya serikali.
“Baada ya tarehe 30 Juni mwaka huu, watoa huduma ambao hawajakamilisha hatua ya kuunganishwa hawataruhusiwa kuendelea kutoa huduma. Lengo letu ni kuondoa mianya ya upotevu wa mapato na kuhakikisha usalama, uwazi, na ufanisi katika utoaji wa huduma kwa abiria,” amesema Pazzy.
Pazzy ametaja kampuni zilizojumuishwa kwenye mfumo huo kuwa ni pamoja na Logix Co Limited, Itule Company Limited, Busbora Company Limited, Duarani Innovate Limited, Web Corporation Tanzania Limited, Hashtech Tanzania Limited, Otapp Agency Company Limited, Sepa Tech Limited, Iyishe Company Ltd - Adventure Connection, Global Light & Company Limited, Mkombozi Infotech Company Limited, Meerkatz - Kidia One, Abood Bus Services, Borita Company Limited, na Exabytes Africa Ltd.
Ameongeza kuwa LATRA, kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, inaendelea na ukaguzi wa mabasi ya abiria nchi nzima. Ukaguzi huo unahusisha uhakiki wa leseni za usafirishaji, matumizi ya mikanda ya usalama, uwekaji wa alama kwenye mizigo ya abiria, na ufuatiliaji wa matumizi sahihi ya tiketi za kielektroniki.
Katika hatua nyingine, LATRA imeonya kuwa wahudumu wa mabasi ambao hawajasajiliwa na mamlaka hiyo hawataruhusiwa kuendelea na kazi, na hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wakiukaji.
“Wahudumu wote wanapaswa kuwa wamepata mafunzo kutoka vyuo vinavyotambulika kama Chuo cha Ufundi Arusha (ATC), Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT). Aidha, wanapaswa kuwa na vitambulisho rasmi na kutoa huduma kwa nidhamu, usafi, na staha kwa abiria,” ameongeza.
Kwa mujibu wa LATRA, baadhi ya makosa ya mara kwa mara yanayofanywa na wahudumu ni pamoja na kuweka muziki usiofaa, kuruhusu biashara holela ndani ya mabasi, na kushindwa kudhibiti mizigo ya abiria.
Wahudumu wa mabasi kwa upande wao wamepongeza hatua hiyo ya ukaguzi ikielezwa kuwa inawakumbusha wajibu wao na inasaidia kuboresha huduma kwa abiria wakati wote wa safari.
#KhomeinTvUpdates
✍️Mwandishi wetu
PIA USIACHE KU SUBSCRIBE
CHANEL YETU Khomein TV
YOUTUBE UWE WA KWANZA
KUFIKIWA NA HABARI ZETU
Follow Insta & Threads @khomeintv_
Tufollow pia kwenye X (Twitter), TikTok
@khomeintv na Facebook Khomein Tv
0 Comments