Katika kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, za kuwawezesha vijana kiuchumi na kijamii, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imekabidhi rasmi Cheti cha Uwakala kwa Chama cha Ushirika cha Kuweka na Kukopa cha Maafisa Usafirishaji wa Pikipiki Dar es Salaam (MAUPIDA SACCOS LTD).
Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika Agosti 13, 2025 katika Ukumbi wa Golden Jubilee jijini Dar es Salaam, ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila.
Mpogolo amepongeza jitihada za LATRA katika kuratibu na kutambua mchango wa vijana wanaojiajiri kupitia usafirishaji wa abiria kwa pikipiki. Aidha, amewahimiza maofisa usafirishaji kufuata sheria na kanuni za usalama barabarani kwa manufaa ya jamii na uchumi wa Taifa.
“LATRA wametuheshimisha zaidi na zaidi. Sasa tunaanza kuonekana kama vijana tunaopambana kuelekea uchumi wa kujitegemea. Cheti hiki kinatupa taswira chanya,” amesema Mpogolo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usafiri Barabarani kutoka LATRA, DCP Johansen Kahatano, amesema lengo la kukabidhi cheti hicho ni kuwawezesha vijana kwa kuwapa fursa ya kujiendesha kiuchumi kupitia mfumo rasmi wa uwakala wa usafirishaji.
“Tunaamini kupitia ushirika wenu huu, mtakuza mitaji na uchumi wenu. Mnaweza kukopeshana ndani kwa ndani na kuendeleza kazi yenu ya usafirishaji,” amesema DCP Kahatano.
Aidha, DCP Kahatano amesisitiza kuwa uwepo wa SACCOS hiyo utawasaidia wanachama kuepuka mikopo kandamizi isiyo rafiki, huku akisisitiza umuhimu wa kuwa na mifumo ya ndani ya kifedha yenye kuaminika na isiyowaumiza.
“Kama kauli mbiu yenu inavyosema, ‘SACCOS ni Suluhisho la Mtaji’, basi na nyie mkopeshane wenyewe ndani kwa ndani ili kuepuka mikopo ya kausha damu,”.
Kupitia mpango huu, LATRA inaendeleza dhamira ya serikali ya awamu ya sita ya kuwajengea uwezo wananchi kupitia vyama vya ushirika, ikiwa ni sehemu ya maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha uchumi shirikishi na jumuishi.
#KhomeinTvUpdates
✍️Mwandishi wetu
PIA USIACHE KU SUBSCRIBE
CHANEL YETU Khomein TV
YOUTUBE UWE WA KWANZA
KUFIKIWA NA HABARI ZETU
Follow Insta & Threads @khomeintv_
Tufollow pia kwenye X (Twitter), TikTok
@khomeintv na Facebook Khomein Tv
0 Comments