WAOMBA KUONDOLEWA VIKWAZO BIASHARA YA MAZAO YA KILIMO IKOLOJIA MIPAKANI

 

SERIKALI katika nchi za Afrika ya Mashariki, zimeombwa kuondoa vikwazo ambavyo vinaathiri biashara za mipakani za mazao ya kilimo Ikololojia, hasa kwa wajasiriamali wadogo ili kuwezesha kukuza biashara hiyo.

 

Utafiti uliofanywa kuhusiana na biashara za kilimo Ikolojia (Kilimo Hai) mipakani zimebaini kuna changamoto kadhaa ikiwepo viwango vya ubora wa bidhaa,mifumo ya ulipaji kodi,vikwazo vya barabarani,udhibiti wa bidhaa zisizo na ubora na uelewa mdogo wa wajasiriamali katika masuala ya biashara ya mipakani.

 

Akisoma mapendekezo ya kisera kutokana na  warsha ya wadau kuhusu biashara  ya mipakani kwa mazao ya bidhaa za kilimo Ikolojia, Afisa wa utetezi na ushawishi wa shirikisho la  wakulima Tanzania (SHIWAKUTA), Thomas Laizer amesema   wamekubaliana ni  muhimu, kuchukuliwa kwa hatua madhubuti kuondoa au kupunguza  vikwazo visivyo vya kikodi (NTBs) ikiwemo mazuio yasiyo rasmi ya barabarani ambayo kwa kiasi kikubwa inaathiri biashara za mipakani (cross-border trade).  

 


Laizer ameaema vikwazo hivyo  sio tu  vinavuruga mfumo wa kibiashara, bali unamuumiza mkulima kwani wafanyabiasha huishia kununua mazao kwa bei ya chini kufidia hasara wanayoitarajia kukumbana nayo wasafirishapo mazao. 

 

"Hali hii huchochea wafanyabiashara na wazalishaji kutumia njia zisizo rasmi (njia za panya) kusafirisha mazao na bidhaa na hivyo kukosesha serikali mapato ambayo huyatumia kuwaletea wananchi maendeleo," amesema.

 

Amesema pia wanapendekeza Serikali na wadau, kuchukua hatua ya kuwekeza katika kuwaelimisha wakulima kuhusu mahitaji ya kisera na kisheria yanayohusu uzalishaji wa mazao na bidhaa za kilimo ikolojia ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika biashara za mipakani (cross-border trade) na kukuza uchumi wa kilimo endelevu.

 

Laizer amesema pia wanahimiza Serikali  kuchukua jukumu la msingi katika kuweka miundombinu wezeshi, sera rafiki na mikakati shirikishi ili kuwawezesha Watanzania kufikia masoko ya kimataifa kwa bidhaa ghafi na zilizosindikwa, hivyo kuongeza thamani ya mazao na kukuza pato la Taifa.

 

"Tunatambua na kukubali kuwa uwepo wa wanunuzi na wafanyabiashara toka nje ni fursa kwa wazalishaji wadogo nchini na  Tunatoa wito kwa serikali yetu kuweka mazingira wezeshi na ya uwazi yatakayolinda maslahi ya wazalishaji wa ndani kwa kuhakikisha biashara inayoendeshwa inanufaisha wazalishaji hao, inazingatia haki na usawa, na serikali inapata mapato stahiki ili kuweza kuwaletea wananchi wake maendeleo," amesema.

 

Laizer amesema wamekubaliana Serikali ya Tanzania inapaswa kuzijengea uwezo wa kirasilimali, ikiwa ni pamoja na rasilimali watu na vifaa, mamlaka zinazodhibiti ubora wa mazao ili ziweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuhakikisha walaji wanalindwa dhidi ya mazao yaliyozalishwa kwa kutumia pembejeo zenye viambata hatarishi kwa afya na mazingira.

 

Amesema wanapendekeza  Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kutumia nafasi yake kuzihimiza nchi wanachama kuweka sera na mikakati ya pamoja itakayoielekeza Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuwa ukanda wa uzalishaji na biashara ya mazao na bidhaa zilizozalishwa kiikolojia, kwa lengo la kulinda afya ya walaji, kuhifadhi mazingira, na kuongeza ushindani wa bidhaa za ukanda huu katika masoko ya kikanda na kimataifa.

 

Awali wakizungumzia Utafiti huo, uliofanywa na washauri wa biashara za kilimo Ikolojia mpakani, kwa udhamini wa  Shirika la Muungano wa Uhuru wa chakula Afrika (AFSA), Afisa Miradi wa SHIWAKUTA na MVIWAARUSHA, Damian Sulumo  amesema kama vikwazo vya biashara ya mazao ya kilimo Ikolojia vikiondolewa uzalishaji utaongezeka.

 

Sulumo amesema hata hivyo, bado kunahitajika mafunzo kwa wafanyabiashara wa bidhaa za kilimo Ikolojia  ili kuboresha bidhaa zao na badala kuendelea kuuza nje bidhaa kama  malighafi wanatakiwa kuuza bidhaa zilizosindikwa katika masoko ya kimataifa.

 

Mshauri wa biashara za mazao ya Kilimo Ikolojia wa AFSA , Africa Kiiza  ambaye aliongoza utafiti huo, amesema anaamini mapendekezo ambayo wametoa baada ya utafiti huo, yatakwenda kufanyiwa kazi.

 

Amesema AFSA kwa kushirikiana na wadau wengine, itaendelea kuwajengea uwezo wadau mbalimbali, ikiwepo wabunge wa EAC,wanahabari  na wafanyabiashara wamazao ya kilimo Ikolojia.

 

Mratibu wa SHIWAKUTA  Richard Masandika , amesema utafiti huo uliofanyika katika mipaka ya  Tanzania na Kenya, Kenya na Rwanda na nchi mipaka mingine katika nchi za Afrika ya Mashariki, umekuwa na manufaa makubwa.

 

Amesema wanaimani kuna taratibu za kikanda na kiserikali za EAC, zinaweza kufanywa ili kuondoa vikwazo kwa wafanyabiashara wa bidhaa za kilimo Ikolojia.

 

Wadau wa kilimo Ikolojia katika nchi za Afrika ya Mashariki, wakiwepo wakulima, vyama vya wakulima, watafiti na wanahabari za kilimo Ikolojia walishiriki warsha ya siku mbili jijini Arusha, kuhusiana na utafiti uliofanywa wa AFSA  kuhusiana na biashara za kilimo Ikolojia (Kilimo Hai) mipakani

 

#KhomeinTvUpdates 

 

✍️Mwandishi wetu-Arusha

 

PIA USIACHE KU SUBSCRIBE

CHANEL YETU Khomein TV

YOUTUBE UWE WA KWANZA 

KUFIKIWA NA HABARI ZETU

 

Follow Insta & Threads @khomeintv_

Tufollow pia kwenye X (Twitter), TikTok

@khomeintv na Facebook Khomein Tv

Post a Comment

0 Comments