SERIKALI YAPUNGUZA VIFO VYA UZAZI KWA 18% NYANDA ZA JUU KUSINI MAGHARIBI

 

Jitihada zinazofanywa na Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, zinaendelea kuonekana, kwa Serikali kufanikiwa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kwa asilimia 18,  kutoka vifo 121 kwa vizazi hai 100,000 kwa mwaka 2021 hadi kufikia vifo 83 kwa vizazi hai 100,000 mwaka 2023 katika Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini Magharibi.

 

Taarifa hiyo imetolewa Disemba 12, 2024 na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya Dkt. Godlove Mbwanji, wakati akifungua Kikao kazi cha kufanya tathimini na kubadilishana uzoefu wa utekelezaji wa njia bora za kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na mtoto kwa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Magharibi, ambayo ni Mikoa ya Mbeya, Songwe na Rukwa.

 

Dkt. Mbwanji amesema kupungua kwa vifo hivyo ni jitihada kubwa  za Uwekezaji uliofanywa na Serikali ya awamu ya Sita, katika miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia katika miundombinu, vifaa na vifaa tiba vya kisasa pamoja na utendaji kazi bora wa Watumishi wa Sekta ya Afya, kwenye vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini.

 

“Tutumie fursa hii na kutoa pongezi nyingi na shukrani kwa watumishi wa Sekta ya Afya walio chini kwa kujitoa kwao kuwahudumia wananchi bila kujali changamoto wanazokutana nazo,” amesema Dkt. Mbwanji.

 

Ameongeza kuwa, kauli mbiu ya kikao hicho ni “Uongozi na Uwajibikaji ni chachu ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga,” hivyo amewataka viongozi wa hospital zote Mikoa ya Nyanda za juu Kusini Magharibi kutoa uongozi unaozingatia utu na kujali wanaowaongoza.

 

“Ni wajibu wetu kuwa viongozi wenye kujali utu kwa Watumishi wetu na wao wana wajibu wa kuwajibika kutimiza wajibu wao ili sisi sote kwa pamoja tuweze kupata matokeo mazuri zaidi,” amesema Dkt. Mbwanji

 

Awali akitoa salamu za Wizara ya Afya Afisa Programu ya uzazi salama Dkt. Ulimbakisye Macdonald amesema, kazi nzuri inafanyika ndani ya Mikoa ya kupunguza vifo vya mama na mtoto, ni lazima kukumbushana juu ya uwajibikaji kwenye maeneo ya kazi ili kazi hizo nzuri ziendelee kuleta tija kwa Taifa.

 

“Watumishi wenzetu wanafanya kazi kubwa ya kuwahudumia wananchi kila siku na Wizara ya Afya inaunga mkono juhudi zenu, lengo kuu la Rais Dkt. Samia ni kuona hivi vifo havitokei kabisa hivyo kupitia Idara ya mama na mtoto, ameweza kutuunga mkono kwa kuanzisha huduma za kambi ya matibabu ya madaktari.” amesema Ulimbakisye.

 

Kambi hii imeanzishwa baada ya Rais Samia kuona juhudi za kupunguza vifo vya mama na mtoto na hata wananchi wengine kupata huduma za matibabu mengine ikiwepo mafunzo kazi kwa watumishi wa afya.

 

#KhomeinTvUpdates

 

️Mwandishi wetu

 

PIA USIACHE KU SUBSCRIBE

CHANEL YETU Khomein TV

YOUTUBE UWE WA KWANZA 

KUFIKIWA NA HABARI ZETU

 

Follow Insta & Threads @khomeintv_

Tufollow pia kwenye X (Twitter), TikTok

@khomeintv na Facebook Khomein Tv

Post a Comment

0 Comments