Wazee mkoani Mtwara wameiomba serikali kutoa huduma ya msamaha wa matibabu kwa ugonjwa wa Tezi Dume, ambao unatajwa kuwa miongoni mwa maradhi hatarishi kwa wazee.
Wametoa ombi leo Februari 26, 2025 wakiwa kwenye kikao cha Baraza la Wazee wa Mkoa huo, kinachofanyika kwa siku Mbili kwenye ukumbi wa shule ya sekondari ya Mustafa Sabodo, Halmashauri ya wilaya ya Mtwara.
Makamu mwenyekiti wa Baraza hilo, Mzee Rashid Kapela, amesema maradhi ya Tezi Dume huwasumbua wazee walio wengi, na kwamba wengi wao wanakabiliwa na hali duni ya kipato, hivyo kujikuta wengi hupoteza maisha kutokana na kushindwa kumudu gharama za matibabu.
“Kwasababu huu ugonjwa una gharama kubwa, gharama yake ni kwamba unatakiwa ufanye upasuaji, sasa kwa wazee walio wengi uwezo wa kutoa pesa kwa ajili ya kufanya upasuaji hawana.” Amesema mzee Kapela.
Naye mzee Rashid Chilombo, mwakilishi wa wazee wa wilaya ya Nanyumbu anasema “Tezi Dume sasaivi kwa wazee yani karibu ni wengi sana wana tatizo la Tezi Dume kwahiyo ikiwezekana waingizwe msamaha, ili wenye kuugua Tezi Dume hasa wazee basi wapewe misamaha.”
Suala lingine lililozungumzwa na wazee hao, ni kuiomba serikali kuwapa mikopo ya asilimia 10, kama makundi mengine maalumu ya Wanawake, Vijana na Wenye ulemavu.
Akizungumzia suala la msamaha wa matibabu, mratibu wa Bima ya Afya ya Jamii (ICHF) Halmashauri ya wilaya ya Mtwara John Kavishe, anasema utaratibu wa msamaha kwa wazee kwa sasa hutolewa kupitia barua za utambulisho, na sio kadi kama ilivyokuwa awali.
“Msamaha unatibu aina ya tatizo alilokuwa nalo mzee kwa wakati huo, kama ni Tezi Dume, kama ni tatizo gani kuanzia ngazi ya hospitali ya Zahanati hadi hospitali ya Rufaa ya Taifa, ndio maana kila hospitali ina ofisa ustawi wa jamii.” Kavishe.
Akifungua kikao hicho kwa niaba ya Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Ofisa Tarafa ya Mikndani Tito Cholobi, akasisitiza wazee kujikita kwenye shughuli za uchumi.
“Uchumi wa huku Mtwara huku wanaouendesha ni wazee..ukizungumza mashamba ya mikorosho tuliyonayo kuna kijana ana shamba la mikorosho?..ni wachache, na kama wanayo basi ni ya kurithi na kinachoitwa wachache ni kwasababu wamekuwa na moyo hawajayauza. Kuna watu mkiwaachia tu anapiga baei, kwahiyo tukifundishwa uchumi la kwanza ni wakwetu sisi lakini la pili tuwafundishe hawa watoto wetu.” Amesisitiza Cholobi.
Kikao hicho cha Baraza la wazee kinafanyika kwa siku Mbili, ambapo kinatarajia kufanya uchaguzi wa kujaza nafasi ya mwenyekiti wa Baraza wa Mkoa, ambayo ipo wazi baada ya aliyekuwepo awali Meja Mstaafu Mbwana kufariki dunia mwaka jana.
#KhomeinTvUpdates
✍️Juma Mohamed-Mtwara
PIA USIACHE KU SUBSCRIBE
CHANEL YETU Khomein TV
YOUTUBE UWE WA KWANZA
KUFIKIWA NA HABARI ZETU
Follow Insta & Threads @khomeintv_
Tufollow pia kwenye X (Twitter), TikTok
@khomeintv na Facebook Khomein Tv
0 Comments