Wakazi wa Kijiji cha Namtumbuka shuleni, kata ya Namtumbuka halmashauri ya mji Nanyamba mkoani Mtwara, wameomba kukarabatiwa kwa shule yao ya msingi ambayo ni chakavu, wakidai kuwa inakabiliwa na uhaba wa madawati hali inayopelekea baadhi ya watoto kukaa chini.
Wamezungumza hayo kijijini hapo mbele ya Mbunge wa Nanyamba Abdallah Chikota, ambaye amefika kufanya mkutano wa hadhara kueleza utekelezaji wa miradi mbalimbali pamoja na kupokea kero za wananchi.
Said Chilambo na Omary Pesa Pinda, ni miongoni mwa wakazi wa Kijiji hicho ambao wamepaza sauti kuwasilisha kero zilizopo kwenye shule hiyo, inayodaiwa kuwa imejengwa miaka ya 1970.
“Bati juu pale zimetobokatoboka hata kama ikinyesha mvua wanafunzi wanalowa, halafu linalofuata hata sehemu ya kukaa watoto yanakuwa na mushkiri ni wengi wanakaa chini tu, benchi lile halipo (Akimaanisha madawati).” Ameeleza Said Chilambo.
Naye Omary Pesa Pinda anasema “wapo watoto wanakaa chini ndio, mvua ikinyesha mabati yale yametobokatoboka yameoza yani inatia aibu.”
Mtendaji wa kijiji, Jafari Mkuchi, anasema shule yao ina jumla ya wanafunzi 556, huku ikiwa na madawati 80 pekee, na walimu waliopo ni Wanne, ambapo kati yao mmoja anatarajia kustaafu mwezi huu wa Machi mwaka huu.
“Wanaokaa kwenye madawati ili wakae wote yani takriabani wakae watoto Wanne au Watano kwa dawati moja, ndio inaweza kufikia uwiano wa watoto wale.” Amesema Mkuchi.
Mbunge wa Nanyamba Abdallah Chikota, amekutana na kero hiyo kijijini hapo wakati akifanya mkutano wa hadhara, kisha akatoa majibu juu ya utatuzi wa changamoto za shule hiyo, hususani uhaba wa walimu na uchakavu wa majengo.
“Itakapofika fedha ya ukarabati wa Namtumbuka shuleni, ile shule itakarabatiwa kwasababu tunaenda awamu kwa awamu, tumekarabati Likwaya juzi nilikuwa hapo Mnongodi tumefanya ukarabati mkubwa wa madarasa kama sita hivi sasa wanakwenda vizuri, tumefanya Nitekela, tumejenga Chawi, tumejenga Nyundo na maeneo mengine tunajenga.” Amesema Chikota.
Kaimu Ofisa elimu Msingi wa halmashauri ya mji Nanyamba Deus Mkumbo, amesema hatua walizoanza kuzichukua katika shule hiyo, ni pamoja na kupeleka fedha shilingi Milioni 12 kwa ajili ya kuanza ukarabati, lakini baadaye watapeleka tena shilingi Milioni 36, na kufanya jumla ya shilingi Milioni 48.
#KhomeinTvUpdates
✍️ Juma Mohamed-Mtwara
PIA USIACHE KU SUBSCRIBE
CHANEL YETU Khomein TV
YOUTUBE UWE WA KWANZA
KUFIKIWA NA HABARI ZETU
Follow Insta @khomeintv_
Tufollow pia kwenye X (Twitter), TikTok
@khomeintv na Facebook Khomein Tv
0 Comments