WAISILAMU MTWARA WATAKIWA KUTUMIA IBADA ZA IJUMAA KUOMBA UCHAGUZI MKUU UPITE KWA AMANI TZ

 

Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Jamaldin Chamwi, amewataka waumini wa Kiisilamu mkoani humo kutumia ibada za kila Ijumaa, kuliombea Taifa la Tanzania kufanikisha uchaguzi Mkuu ujao mwezi Oktoba mwaka huu, uwe wa amani na utulivu.

 

Sheikh Chamwi, amezungumza hayo Machi 29, 2025 mjini Mtwara, wakati wa hafla ya dua maalumu ya kumuombea kheri Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, sambamba na taifa la Tanzania kwa ujumla, iliyoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala na kufanyika katika viwanja vya Mashujaa Manispaa ya Mtwara-Mikindani.

 


“Tumuombe Mwenyezimungu atupitishe salama katika uchaguzi wetu mkuu ujao, tujitahidi ndani ya hotuba za Ijumaa tusiseme imetosha, tuendelee na kuwakumbusha waisilamu na jamii kwa ujumla na kumuomba Mwenyezimungu Subhannahu-wataallah atuvushe salama katika vuguvugu la uchaguzi linalokuja.” Amesisitiza Sheikh Chamwi.

 

Naye Makamu Askofu wa Kanisa Kuu Jimbo Katoliki Mtwara, Padre Patrick Mwaya, amesema “ni nafasi ya pekee kutumia fursa hii ya utulivu na amani tuliyonayo kuweza kuwachagua viongozi wanaostahiki kusudi waendelee kudumisha, kulinda na kutuongoza kwa amani katika Taifa letu.” 

 

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala, akihutubia kwenye hafla hiyo, akawataka wakazi wa mkoa huo kuendeleza amani iliyopo, huku akiwataka kutoyaunga mkono makundi yatakayojitokeza kipindi hiki kuelekea uchaguzi Mkuu, yenye lengo la kuvura amani.

 


“Kila mmoja asikubali kwa namna yoyote, kuchafua amani na utulivu wa nchi yetu. Hakuna utakapokimbilia zaidi ya Tanzania, wote tunasikia huko watu wanavyopata tabu, maeneo mbalimbali ambapo hakuna utulivu, tunaombeni sana amani na utulivu ambao upo ndani ya nchi yetu ambayo inatuwezesha sasa hivi Wanamtwara kukaa pamja sasa hivi tukimshukuru Mwenyezimungu, tuendelee kuidumisha, tuidumishe amani hii na yeyote atakayependa kuichezea msikubaliane naye.” Ameonya Kanali Sawala.


Kwa upande wake, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mtwara Ibrahim Mjanakheri Ibrahim, ameunga mkono kauli za viongozi wa dini pamoja na mkuu wa Mkoa, juu ya kuilinda amani iliyopo.

 

#KhomeinTvUpdates 

 

✍️Juma Mohamed-Mtwara

 

PIA USIACHE KU SUBSCRIBE

CHANEL YETU Khomein TV

YOUTUBE UWE WA KWANZA 

KUFIKIWA NA HABARI ZETU

 

Follow Insta & Threads @khomeintv_

Tufollow pia kwenye X (Twitter), TikTok

@khomeintv na Facebook Khomein Tv

Post a Comment

0 Comments