Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Juni 25, 2025 ameshiriki maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Jamhuri ya Msumbiji, akitoa salamu za pongezi kwa Taifa hilo ndugu na kusisitiza dhamira ya kuendeleza uhusiano wa kihistoria, kindugu, na kiuchumi kati ya Mataifa haya mawili jirani.
Katika hotuba yake, Rais Samia alikumbusha mchango mkubwa wa Tanzania katika harakati za ukombozi wa Msumbiji, ambapo nchi ilitoa hifadhi kwa wapigania uhuru wa FRELIMO walioweka kambi zao katika maeneo ya Bagamoyo (Pwani), Kongwa (Dodoma), na baadaye Nachingwea (Lindi). Amesema historia hiyo ni kielelezo cha mshikamano wa kweli uliokuwepo wakati wa mapambano na unaoendelea hadi leo.
"Sisi ni ndugu, hivyo uhuru wao ni uhuru wetu", amesisitiza Rais Samia, akionyesha fahari ya mchango wa Tanzania katika kusaidia kuifikia siku hii ya kihistoria.
Aidha, Rais Samia amewapongeza wananchi na serikali ya Msumbiji kwa mafanikio makubwa waliyoendelea kuyapata katika nyanja mbalimbali, ikiwa ni pamoja na maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Ameeleza kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya juhudi za pamoja, mshikamano, na uongozi madhubuti.
Rais Samia amesisitiza kuwa Tanzania itaendelea kudumisha na kuimarisha ushirikiano wa karibu na Msumbiji, si tu kwa misingi ya historia, bali kwa lengo la kufanikisha azma ya pamoja ya kujenga jamii zenye usawa, haki, na maendeleo endelevu kwa watu wa Mataifa yote mawili.
"Tutaendelea kudumisha na kuimarisha ushirikiano huu ili kuifikia azma ya uhuru wa nchi zetu, ambayo ni kujenga jamii yenye usawa na kuchochea maendeleo ya wananchi wetu," amesema.
Maadhimisho haya ni ishara ya mafanikio ya muda mrefu wa ukombozi wa bara la Afrika, na yanatoa fursa kwa Mataifa ya Afrika kuenzi historia yao ya kupigania uhuru, huku yakiweka mbele ajenda za maendeleo na mshikamano wa kikanda.
#KhomeinTvUpdates
✍️Mwandishi wetu
PIA USIACHE KU SUBSCRIBE
CHANEL YETU Khomein TV
YOUTUBE UWE WA KWANZA
KUFIKIWA NA HABARI ZETU
Follow Insta & Threads @khomeintv_
Tufollow pia kwenye X (Twitter), TikTok
@khomeintv na Facebook Khomein Tv
0 Comments