Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeibuka kidedea kwa kushika nafasi ya kwanza katika utoaji wa huduma bora kwa wateja mkoani Lindi, katika Maonesho ya Madini (Mining Expo 2025) yaliyofanyika Wilayani Ruangwa.
Tuzo hiyo ya heshima imekabidhiwa na Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, na kupokelewa kwa niaba ya shirika na Kaimu Meneja wa TANESCO mkoa wa Lindi, Theodory Hall. Ambapo ushindi wa pili ulikwenda kwa Kampuni ya Madini ya Eliange na ushindi wa tatu kwa T ONE Mable, watengenezaji wa marumaru inayotokana na madini kutoka mkoani Lindi.
Maonesho haya makubwa yaliyoandaliwa na Wizara ya Madini yalianza rasmi Juni 11 na kufikia kilele chake Juni 14, 2025, yakilenga kuwakutanisha wadau wa sekta ya madini wakiwemo wachimbaji wakubwa na wadogo, wawekezaji, taasisi za umma na binafsi, pamoja na wananchi.
Katika maonesho hayo, TANESCO ilitumia fursa hiyo kuonyesha kwa vitendo mafanikio na utekelezaji wa miradi yake ya kimkakati katika uzalishaji, usambazaji na upatikanaji wa nishati ya umeme nchini. Vilevile, wananchi walipata elimu kuhusu matumizi salama ya umeme, upatikanaji wa huduma mbalimbali, na kuhamasishwa kuhusu matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia, hatua muhimu katika kulinda mazingira na afya za watumiaji.
Ushiriki wa TANESCO kwenye maonesho haya ni kielelezo cha dhamira ya dhati ya Shirika hilo ya kutoa huduma bora, za kisasa na zenye kuwafikia wananchi wote. Ushindi huu unaonesha pia mchango mkubwa wa TANESCO katika kuimarisha sekta ya madini kupitia nishati endelevu inayochochea ukuaji wa viwanda na uwekezaji.
Serikali kwa kushirikiana na wadau kama TANESCO inaendelea kutekeleza mkakati wa kukuza sekta ya madini kwa tija, kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.
Hongera TANESCO – Huduma Bora ni Kielelezo cha Uzalendo na Ufanisi!
#KhomeinTvUpdates
✍️Mwandishi wetu
PIA USIACHE KU SUBSCRIBE
CHANEL YETU Khomein TV
YOUTUBE UWE WA KWANZA
KUFIKIWA NA HABARI ZETU
Follow Insta & Threads @khomeintv_
Tufollow pia kwenye X (Twitter), TikTok
@khomeintv na Facebook Khomein Tv
0 Comments