Nikiwa miongoni mwa Watanzania walioshtushwa na uamuzi wa Ndugu Humphrey Polepole kujiuzuru nafasi yake ya Ubalozi nchini Cuba, nilitamani sana kufahamu kipi hasa kilimsibu mpaka kufikia kuchukua uamuzi ule mzito?
Baada ya kumsikiliza kwa kina Ndugu Polepole nilijiuliza swali moja kubwa kichwani; Ndugu Polepole anaijua Katiba aliyoitaja?
Kwa nini nasema hivi? Kwa sababu katika mazungumzo yake Ndugu Polepole alisikika akisema kuwa mara baada ya kufariki kwa Rais aliyepo madarakani uchaguzi ulitakiwa kuitishwa kwa haraka. Hili si kweli! Nasikitika kusema kuwa amedanganya umma, sijui ni kwa bahati mbaya au kwa makusudi!?
Hapa ndipo linapokuja swali kuu lililo katika kichwa cha hoja kwamba, "Polepole amesema kweli au kuna ajenda imejificha nyuma yake?
Katika kutabanaisha hili ni vema tuweke vifungu vya Katiba ambavyo Ndugu Polepole labda hakuvinukuu kwa bahati mbaya au labda kwa makusudi ili kukidhi haja ya hoja yake.
Hivyo tutazame Ibara ya 37 ibara ndogo ya 5 ya Katiba inasemaje?
Ibara ya 37 (5) inasema; "Endapo kiti cha Rais kitakuwa wazi kutokana na Rais kufariki dunia, kujiuzulu, kupoteza sifa za uchaguzi au kutomudu kazi zake kutokana na maradhi ya mwili au kushindwa kutekeleza kazi na shughuli za Rais, basi Makamu wa Rais ataapishwa na atakuwa Rais kwa muda uliobaki katika kipindi cha miaka mitano na kwa masharti yaliyoelezwa katika ibara ya 40, kisha baada ya kushauriana na chama cha siasa anachotoka Rais atapendekeza jina la mtu atakae kuwa Makamu wa Rais na uteuzi huo utathibitishwa na Bunge kwa kura zisizopungua asilimia hamsini ya Wabunge wote."
Tujiulize Katiba imesema ufanyike uchaguzi au Makamu wa Rais ataapishwa na atakuwa Rais kwa muda uliobaki?
Ni Katiba ipi aliyoisoma Ndugu Polepole ambayo ina Ibara tofauti na hii?
Aidha, tutazame Ibara ya 40 ambayo imeainishwa katika ibara ya 37 ibara ndogo ya 5. Hapa tutazame Ibara ndogo ya 4 ambayo kimsingi ndiyo inafafanua ibara ya 37 Ibara ndogo ya 5:
Ibara ya 40 (4) inasema; "Endapo Makamu wa Rais anashika kiti cha Rais kwa mujibu wa masharti ya ibara ya 37(5) kwa kipindi kinachopungua miaka mitatu ataruhusiwa kugombea nafasi ya Rais mara mbili, lakini kama akishika kiti cha Rais kwa muda wa miaka mitatu au zaidi ataruhusiwa kugombea nafasi ya Rais mara moja tu."
Je Ndugu Polepole hakuisoma Ibara hii pia au kuna ajenda imejificha?
Mbali na Ibara hizo, Ndugu Polepole amezungumzia suala la desturi kwamba licha ya uwepo Katiba, CCM ina desturi yake kwamba yule atakayekuwa Makamu wa Rais, Spika au Waziri Mkuu hawezi kugombea tena Urais.
Hapa nadhani Ndugu Polepole kuna kitu ameshindwa kutambua au kukumbuka; kwamba mara baada ya kufariki kwa Hayati Magufuli, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliapishwa kuwa Rais, hivyo desturi aliyoisema hapo haikidhi kwa Rais Samia kwa mujibu desturi anayoisema bali inawahusu Makamu wake wa Rais, Waziri Mkuu wake na hata Spika.
Lakini pia katika hilihili la desturi Ndugu Polepole alizungumzia mchakato wa kumpata mgombea wa Urais ndani ya CCM na kuukosoa, kwamba kwa mujibu wake ulipaswa uanze upya.
Lakini jambo la kustaajabisha hapa ni kwamba Ndugu Polepole alikuwa Mwenezi katika kipindi ambacho uchaguzi ndani ya CCM ulivurugwa mno, ina maana Ndugu Polepole leo hii amesahau kuwa akiwa Mwenezi wale walioongoza katika kura za maoni waliondolewa na kuwekwa wagombea wengine ndani ya Chama?
Sambamba na hilo, katika maelezo yake alienda mbali na kunukuu kitabu cha TANU/CCM na Watu, kwamba watu waheshimiwe. Je katika hili la kuwapangia mgombea ubunge watu yeye akiwa Mwenezi hakuona kuwa ni uhuni?
Mbona hatukumsikia akisema lolote? Ni utaratibu gani anaozungumzia ikiwa yeye mwenyewe alikuwa sehemu ya kuvuruga utaratibu kipindi akiwa Mwenezi? Je hapa nani muhuni, kama si yeye mwenyewe?
Je mwaka 2020 mgombea wa CCM alishindanishwa ndani ya chama kama anavyotaka Ndugu Polepole hivi sasa? Hakuliona hili wakati ule akiwa Mwenezi?
Hapa ndipo ninapopata mashaka kuwa labda Ndugu Polepole ana ajenda ya siri illiyojificha katika hiki alichodai ni maelezo ya yeye kujiuzuru Ubalozi.
Katika maelezo yote aliyotoa Ndugu Polepole, kwa mtu mwenye kufikiri vema atabaini kuwa Ndugu Polepole anachopinga ni Mhe. Rais Samia kutetea nafasi yake ya Urais kwa mujibu wa Katiba. Hii ndiyo ajenda ambayo imejificha nyuma ya maelezo yote yaliyochukua takribani saa mbili. Ina maana ana mgombea wake ambaye alitaka awe Rais, je ni yupi?
#KhomeinTvUpdates
✍️Mwandishi wetu
PIA USIACHE KU SUBSCRIBE
CHANEL YETU Khomein TV
YOUTUBE UWE WA KWANZA
KUFIKIWA NA HABARI ZETU
Follow Insta & Threads @khomeintv_
Tufollow pia kwenye X (Twitter), TikTok
@khomeintv na Facebook Khomein Tv
0 Comments