Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi Prof. Godius Kahyarara ameitaka Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), kuhakikisha wamiliki wa mifumo ya Tiketi Mtandao nchini wanaunganisha mifumo yao na Mfumo Jumuishi wa Mauzo ya Tiketi unaofahamika kwa jina la Safari Tiketi kwa kuwa ni jambo la kisheria na Kikanuni.
Hayo ameyasema alipotembelea jengo la LATRA katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) Dar es Salaam Julai 05, 2025, na kusisitiza kuwa, uunganishaji wa mifumo ya tiketi mtandao na Mfumo Jumuishi wa Serikali ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Nakumbuka Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipokuwa akizindua treni ya kisasa pale Dodoma, alitoa maelekezo nane na mojawapo ni hili la kuwa na Mfumo Jumuishi wa Tiketi Mtandao. Tunafurahi kwamba LATRA wameliwezesha hili na mfumo huu unamwezesha abiria kukata tiketi za mabasi pamoja na treni za kisasa (SGR) na za reli ya kati (MGR) kwa urahisi kwa njia ya mtandao,”amesema Prof. Kahyarara.
Aidha Prof. Kahyarara ameongeza kuwa, mfumo wa Safari Tiketi si tu unarahisisha huduma kwa abiria, bali pia unawawezesha wamiliki wa mabasi kupata mapato yao papo hapo, kufuatilia mabasi yao na kupata takwimu sahihi za abiria wanaosafiri.
Kwa upande wake, CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu LATRA amesema ni kosa kisheria kuwa na mfumo wa kutoa tiketi mtandao bila kuthibitishwa na LATRA, pia, ametoa tahadhari kwa wamiliki wa mabasi kutotumia kampuni za tiketi mtandao zisizoidhinishwa na LATRA baada ya Julai 14, 2025.
“Wamiliki nawatahadharisha msije mkaingia kwenye matatizo ya kuzuiliwa kutoa huduma kwa kuwa usipotoa tiketi mtandao, huruhusiwi kufanya kazi ya usafirishaji na pia haturuhusiwi kukupa leseni. Tumewapa taarifa za awali kuhusu kampuni ambazo hazijakamilisha utaratibu kwahiyo muwafuatilie na muhakikishe mnatumia kampuni zilizokidhi vigezo mara baada ya muda waliopewa kuisha,” amesisitiza CPA Suluo.
#KhomeinTvUpdates
✍️Mwandishi wetu
PIA USIACHE KU SUBSCRIBE
CHANEL YETU Khomein TV
YOUTUBE UWE WA KWANZA
KUFIKIWA NA HABARI ZETU
Follow Insta & Threads @khomeintv_
Tufollow pia kwenye X (Twitter), TikTok
@khomeintv na Facebook Khomein Tv
0 Comments