Uhusiano mzuri wa Tanzania kimataifa umeijengea taswira nzuri ambapo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika miaka minne ya utawala wake, amezidi kuifungua nchi kwa kuonyesha ushirikiano na mataifa mbalimbali, kuutangaza utalii na kukaribisha wawekezaji kuja kuwekeza nchini.
Aidha, Tanzania imezidi kung'ara katika nyanja mbalimbali na kwa kuthibitisha hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Italia (SACE), Bi. Alessandra Ricci ameithibitishia kuwa miongoni mwa nchi 14 za Afrika zitakazonufaika na usaidizi wa kifedha kutoka nchi hiyo.
Hayo yamejiri hivi karibuni mjini Rome nchini Italia wakati Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi huyo, kutokana na uhusiano mzuri wa kiuchumi uliopo kati ya nchi hizo mbili kupitia Mpango wa ushirikiano kati ya Italia na nchi za Afrika ujulikanao kama Piano Mattei.
Dkt. Mwigulu ameishukuru Italia kwa kutoa dhamana ya mkopo wa kujenga Reli ya Kisasa (SGR), kipande cha Kwanza na cha pili kuanzia Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma hadi Makutupora mkoani Singida, ambavyo ujenzi wake umekamilika na treni imeanza kutoa huduma kuanzia Dar es Salaam hadi Dodoma.
Ameeleza kuwa kutokana na mchango huo, SGR imeanza kutoa huduma ya kubeba abiria kuanzia Julai 2024, ikiwa ni mafanikio makubwa katika historia ya usafiri nchini, ambapo muda wa safari kati ya Dar es Salaam na Dodoma umepungua kutoka saa nane hadi saa tatu.
Aidha, Waziri Nchemba ameeleza kuwa Serikali inatambua na kuthamini nia njema ya SACE kuendelea kudhamini ujenzi wa reli toka Dodoma hadi Isaka
Pia, Dkt. Mwigulu amewaalika wawekezaji kutoka Italia kwenda kuwekeza nchini Tanzania katika sekta mbalimbali ikiwemo uendeshaji wa miundombinu ya reli pamoja na ujenzi wa viwanda vitakavyosaidia kukuza ajira na kukuza uchumi wa nchi wa pande hizo mbili.
Amesema kuwa Tanzania iko katika eneo zuri la kimkakati kijiografia kwa kupakana na nchi 6 zisizopakana na Bahari na zinazotegemea Bandari ya Dar es Salaam, hatua ambayo inalifanya eneo lote la nchi na nchi jirani kuwa soko zuri na la uhakika la bidhaa na huduma na kuishauri sekta binafsi ya nchi hiyo kuchangamkia fursa hizo.
#KhomeinTvUpdates
✍️Mwandishi wetu
PIA USIACHE KU SUBSCRIBE
CHANEL YETU Khomein TV
YOUTUBE UWE WA KWANZA
KUFIKIWA NA HABARI ZETU
Follow Insta & Threads @khomeintv_
Tufollow pia kwenye X (Twitter), TikTok
@khomeintv na Facebook Khomein Tv
0 Comments