WAMAREKANI WALIOHUKUMIWA KUNYONGWA DR CONGO WABADILISHIWA ADHABU

 

Wamarekani watatu Marcel Malanga Malu, Tylor Thomson na Zalman Polun Benjamin waliohukumiwa kunyongwa kwa kuhusika katika mapinduzi yaliyofeli nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mwaka jana wamebadilishiwa hukumu za kifo na kuwa kifungo cha maisha jela, ofisi ya rais imesema. 

 

Walikuwa miongoni mwa watu 37 waliohukumiwa kifo Septemba mwaka jana na mahakama ya kijeshi. 

Watatu hao walituhumiwa kuongoza mashambulizi katika ikulu ya rais na nyumba ya mshirika wa Rais Félix Tshisekedi Mei mwaka jana. 

 

Kutenguliwa kwa hukumu hizo kunakuja kabla ya ziara ya mshauri mkuu mpya wa Marekani kuhusu Afrika, Massad Boulos nchini DR Congo.

 

Boulos, baba mkwe wa Binti wa Rais Donald Trump, aitwaye Tiffany, anatarajiwa kuwasili Kinshasa siku ya Alhamisi katika safari ambayo pia itampeleka Rwanda, Kenya na Uganda. 

 

Marekani haijatangaza Wamarekani hao watatu kufungwa kimakosa nchini DR Congo lakini Wizara ya Mambo ya Nje ilisema hapo awali kumekuwa na mazungumzo kati ya nchi hizo kuhusu suala hilo. 

 

Watatu hao walipatikana na hatia ya njama ya uhalifu, ugaidi na mashtaka mengine, ambayo walikanusha. 

Mshukiwa wa kiongozi wa njama hiyo, Christian Malanga, raia wa Marekani mwenye asili ya Congo, aliuawa wakati wa shambulio hilo, pamoja na wengine watano.

 

Kwa jumla watu 51 walihukumiwa katika mahakama ya kijeshi, huku kesi zikitangazwa kwenye TV na redio za kitaifa. 

Watu kumi na wanne waliachiliwa, huku mahakama ikisema hawakuwa na uhusiano wowote na shambulio hilo. 

 

Hukumu za kifo hazijatekelezwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa takribani miongo miwili na wafungwa wanaopokea adhabu hiyo huwa wanatumikia kifungo cha maisha jela. 

 

Siku ya Jumanne, Rais Tshisekedi alitia saini amri za kubatilisha hukumu za kifo za Wamarekani, msemaji wake Tina Salama alisema katika taarifa yake kwenye televisheni. 

Marcel Malanga Malu, Tylor Thomson na Zalman Polun Benjamin - walipewa "huruma ya binafsi," na rais, kulingana na Salama. 

Ckiness Ciamba, mmoja wa mawakili wa Malanga, aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba "msamaha wa rais ni hatua ya kwanza inayoahidi mabadiliko makubwa katika siku zijazo".

 

#KhomeinTvUpdates 

 

✍️BBC Swahili

📸BBC Swahili

 

PIA USIACHE KU SUBSCRIBE

CHANEL YETU Khomein TV

YOUTUBE UWE WA KWANZA 

KUFIKIWA NA HABARI ZETU

 

Follow Insta & Threads @khomeintv_

Tufollow pia kwenye X (Twitter), TikTok

@khomeintv na Facebook Khomein Tv

Post a Comment

0 Comments