RAIS SAMIA AONESHA MASIKITIKO KUFUATIA AJALI MBAYA SAME.

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameonesha masikitiko makubwa kufuatia ajali ya barabarani iliyotokea jana jioni katika eneo la Sabasaba, Barabara Kuu ya Moshi - Tanga, Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, na kusababisha vifo vya watu 37 na majeruhi 30.

 

Kupitia machapisho yake katika mitandao ya kijamii, Rais Samia ameandika:

 

“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya vifo vya ndugu zetu 37 na majeruhi 30 kutokana na ajali ya barabarani iliyotokea jana jioni eneo la Sabasaba, Barabara Kuu ya Moshi - Tanga, Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, kwa magari mawili kugongana na kuungua moto. Ninawaombea kwa Mwenyezi Mungu marehemu wote wapumzike kwa amani, na majeruhi wote wapone kwa haraka. 

 

Ninatoa salamu za pole kwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mheshimiwa Nurdin Babu, familia zote za wafiwa, ndugu, jamaa na marafiki. Mwenyezi Mungu awape faraja na nguvu katika kipindi hiki kigumu.”

 

Katika ujumbe huo, Rais Samia pia amekumbusha maelezo aliyotoa tarehe 27 Juni 2025 katika Hotuba yake ya kuhitimisha shughuli za Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambako alieleza kuwa ajali za barabarani zimeendelea kugharimu maisha ya Watanzania na kuleta majonzi makubwa kwa familia nyingi.

 

Amesisitiza kuwa madereva wanapaswa kuzingatia kwa umakini mkubwa sheria za usalama barabarani, huku akilitaka Jeshi la Polisi kuendelea kusimamia kikamilifu utekelezaji wa sheria hizo ili kulinda maisha ya wananchi.

 

Rais Samia amehitimisha kwa kuwatakia faraja wale wote walioguswa na msiba huo, huku akiweka msisitizo kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua madhubuti za kupunguza ajali na kulinda usalama wa raia wake.

 

#KhomeinTvUpdates 

 

✍️Mwandishi wetu

 

PIA USIACHE KU SUBSCRIBE

CHANEL YETU Khomein TV

YOUTUBE UWE WA KWANZA 

KUFIKIWA NA HABARI ZETU

 

Follow Insta & Threads @khomeintv_

Tufollow pia kwenye X (Twitter), TikTok

@khomeintv na Facebook Khomein Tv

Post a Comment

0 Comments