TANAPA YAIBUKA KIDEDEA TUZO ZA KIMATAIFA ZA WORLD TRAVEL AWARDS

 

 

Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limeibuka mshindi na kufanikiwa kunyakua jumla ya tuzo 7 katika mashindano ya Kimataifa ya World Travel Awards, yaliyofanyika Juni 28,2025,  jijini Dar es Salaam.

 

Tuzo hizo  ni mafanikio makubwa na ya kihistoria ambayo yanaonyesha dhamira thabiti ya TANAPA katika kulinda, kuhifadhi na kukuza utalii wa ndani na wa Kimataifa.

 

TANAPA kupitia hifadhi zake 7 zimeshida tuzo hizo ambapo Hifadhi ya Taifa Serengeti imeibuka mshindi katika tuzo za World Travel Awards katika kipengele cha Hifadhi Bora Barani Afrika (Africa’s Leading National Park), ikiwa ni mara ya saba mfululizo kushinda tuzo hiyo ya kifahari.

 

 Ushindi huu unaonesha ubora na mvuto wa hifadhi hiyo maarufu duniani kwa uoto wake wa asili na uhamaji wa wanyamapori (The Great Migration), jambo linaloendelea kuiweka Tanzania katika ramani ya utalii wa kimataifa.

 

Pia, Hifadhi ya Taifa Mlima Kilimanjaro imetwaa tuzo la Hifadhi Bora ya Milima Barani Afrika (Africa’s Leading Mountain National Park), kutokana na kuwapo kwa mlima mrefu zaidi barani Afrika – Mlima Kilimanjaro ambao huvutia maelfu ya watalii na wapanda milima kutoka kona mbalimbali za dunia.

 

Hifadhi ya Taifa Nyerere nayo haikubaki nyuma, ambapo imeshinda tuzo ya Hifadhi Bora kwa Mandhari ya Kuvutia Barani Afrika (Africa’s Leading Scenic National Park ), ikionyesha jinsi TANAPA inavyoendelea kuhifadhi na kutangaza maeneo yenye thamani ya kitalii na kihistoria.

 

Katika mwendelezo huo, Hifadhi ya Taifa  Tarangire  imeibuka  mshindi katika kipengele cha Hifadhi Bora kwa Utalii wa Tembo, Hifadhi ya Taifa Serengeti kwa mara nyingine kuwa Hifadhi inayoongoza kwa kivutio cha wanyama wakubwa watano (Big Five) , Hifadhi ya Taifa Ruaha kuwa Hifadhi inayoongoza kwa utalii wa kitamaduni Barani Afrika na Hifadhi ya Taifa Kitulo Hifadhi bora kwa fungate Barani Afrika.

 

Ushindi wa hifadhi hizi siyo tu kwamba ni fahari kwa Taifa, bali ni nyenzo muhimu katika kujitangaza kimataifa, kuvutia watalii, na kuongeza mapato ya fedha za kigeni kupitia sekta ya utalii. Tuzo hizi zinaimarisha nafasi ya Tanzania kama kiongozi wa utalii duniani, pamoja na kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt.  Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Kufahamika kwa vivutio hivyo  utatangaza  fursa za uwekezaji nchini, hususan katika maeneo ya  Hifadhi za  Taifa 21 zikizotapakaa kila sehemu ya Taifa la Tanzania

 

#KhomeinTvUpdates 

 

✍️Mwandishi wetu

 

PIA USIACHE KU SUBSCRIBE

CHANEL YETU Khomein TV

YOUTUBE UWE WA KWANZA 

KUFIKIWA NA HABARI ZETU

 

Follow Insta & Threads @khomeintv_

Tufollow pia kwenye X (Twitter), TikTok

@khomeintv na Facebook Khomein Tv

Post a Comment

0 Comments