JIFUNZE HAPA ATHARI ZA KIAFYA ZA GUBU NA KULALAMIKA SANA

 

Katika karne ya 21, ni jambo la kawaida kusikia malalamiko kuhusu msongamano wa magari, hali ya hewa, kazi au ugumu wa kiuchumi. Kwa wengi, ni kitu kisicho na madhara na kinatumiwa kama njia ya kutoa hisia zako.

 

Hata hivyo, malalamiko ya mara kwa mara huwa na athari kubwa kihisia, kisaikolojia, na hata kimwili kwa wale wanaolalamika na wale wanaopokea maneno hayo ya malalamiko.

 

Hapa tutajadili kuhusu kulalamika kila wakati, yaani kutamauka na kutokufurahishwa na hali zinazoonekana kama mbaya. Jambo hili hujitokeza kila mahali, kuanzia katika familia, kazini na hata katika jamii.

Kulalamika mara moja moja ni sehemu ya kawaida kwa binadamu. Lakini athari kwa hisia na mwili hutokea pale malalamiko yanapovamia maisha yetu ya kila siku.

 

Kwa nini tunalalamika sana? Baadhi ya wataalamu wanaamini kulalamika ni njia ya kukabiliana na changamoto, kwa kutoa hisia zetu au kutafuta kukubalika kutoka kwa watu.

Kwa mfano, imedhihirika kwamba kupitia malalamiko tunatafuta maoni yetu au mitazamo yetu ikubalike.

 

Hadi kufikia hapo, malalamiko yanakuwa kama mbinu tu ya kuwasilisha maoni mbele ya kundi la watu na hiyo njia ya kawaida kwa binadamu.

Tatizo huanza pale kulalamika kunapozidi na kuenea katika shughuli za kawaida za maisha.

Tatizo hili linakuwa baya zaidi kutokana na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, ambapo ni jambo la kawaida kwa watu maarufu haswa vijana kutumia sehemu kubwa ya maudhui yao kulalamika kuhusu hili na lile kama mkakati wa kuvutia mashabiki au kuleta mijadala na kubadilishana maoni.

Athari kwa Ubongo na Afya ya Akili

Ingawa ni uwanja unaohitaji utafiti zaidi, lakini sayansi ya mishipa ya fahamu na ubongo tayari imechunguza sababu na athari za kulalamika.

 

Tafiti mbalimbali zinaonyesha kwamba ubongo wa binadamu umeumbwa ili kubaini vitisho na matatizo, jambo linaloeleza kwa nini ni rahisi kuzingatia mambo mabaya na kwa nini watu wengine wana tabia ya kulalamika kuliko wengine.

 

Huu ni mfumo wa kimaumbile. Asili yake ni kwa lengo la kutoa ulinzi: Ubongo hutafuta vitu vibaya ili kukabiliana na hatari halisi na hivyo kufanikiwa kuongeza kuishi kwa muda mrefu.

Lakini jambo hili linaweza kukuharibia katika mazingira ya sasa, kwani kuendelea kuzingatia mabaya kunaweza kubadilisha mtazamo wa watu kuhusu dunia na hivyo kukuza tabia mpya iliojikita kwenye malalamiko.

 

Baadhi ya tafiti zinapendekeza kwamba hali ya kulalamika inaweza kusababisha mabadiliko katika muundo wa ubongo na kusababisha changamoto katika kutatua matatizo na kazi za kiakili.

 

Hii inamaanisha kwamba wale wanaolalamika mara kwa mara wanaweza kushindwa kutatua matatizo, kufanya maamuzi au kupanga. Hii inaharibu mfumo wa maisha zaidi, na hivyo huzalisha malalamiko zaidi.

Zaidi ya hayo, imeonekana kwamba malalamiko ya kila siku yanahusiana na dalili za wasiwasi na msongo wa mawazo.

 

Malalamiko yahusishwa na kufikiria sana, fikra mbaya, kutojithamini, uchovu na uchovu wa kiakili. Kwa sababu hii, watu wanaolalamika kila wakati kuhusu kila kitu mara nyingi huwa na mtazamo hasi na hawana uwezo mzuri wa kupambana na shida.

Mikakati ya Kubadilisha Tabia

Zifuatazo ni baadhi ya njia na mikakati ya kukabiliana na tatizo la kulalamika sana kama zilivyopendekezwa na washauri wa saikolojia:

 

Jifunze kushukuru: Kushukuru kwa kile tulichonacho kunatusaidia kuonesha shukrani. Kuandika mambo tunayoshukuru katika kijitabu kunaweza kusaidia kubadilisha mtazamo wetu.

 

Kutafuta suluhisho: Kutengeneza orodha ya hatua tunazoweza kuchukua kuboresha hali fulani, hilo hutupa hisia ya udhibiti na kupunguza hasira.

 

Zingatia kauli zako: Sayansi inatufundisha kuwa makini na lugha tunayoitumia na kuibadilisha kuwa lugha chanya zaid au ya kati. Hilo linaweza kutusaidia kubadilisha mifumo yetu ya mawazo.

 

Kuweka mipaka: Huu ni mtindo wa kujilinda. Inamaanisha, kwa mfano, kuepuka mazungumzo yanayojikita sana kwenye mambo hasi na badala yake jikite katika mazungumzo ya kujenga.

 

Bila shaka, kutambua tabia hii isiyo ya afya ya kulalamika bila kusita na kujaribu kuibadilisha ni muhimu katika kuboresha maisha.

 

Kabla ya kulalamika tena, fikiria athari kwa akili yako, hisia, na kijamii zinazoambatana na tabia hiyo. Na kumbuka: kulalamika si jambo baya kama si jambo la mara kwa mara. Sisi si wakamilifu, sisi ni binadamu.

 

#KhomeinTvUpdates 

 

✍️BBC Swahili

📸Mtandaoni

 

PIA USIACHE KU SUBSCRIBE

CHANEL YETU Khomein TV

YOUTUBE UWE WA KWANZA 

KUFIKIWA NA HABARI ZETU

 

Follow Insta & Threads @khomeintv_

Tufollow pia kwenye X (Twitter), TikTok

@khomeintv na Facebook Khomein Tv

Post a Comment

0 Comments